Wajumbe wa Kamati ya Usalama ya Wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi, wamesema wilaya hiyo ni miongoni mwa wilaya ambazo wananchi wake wamekuwa wakitii utawala unaozingatia sheria za nchi na masuala ya haki za binadamu, jambo linalopelekea kupungua kwa kiasi kikubwa matukio ya uvunjifu wa amani na ukiukwaji wa haki za binadamu.
Mkuu wa wilaya hiyo Hassan Ngoma, ambaye amefungua mafunzo ya elimu ya Uraia na Utawala Bora kutoka wizara ya Katiba na Sheria, amesema licha ya kuimarika kwa usalama kwa wilaya ya Ruangwa, lakini mafunzo hayo ni muhimu kwao kutokana na utekelezaji wa majukumu yao.
“Ni muhimu kundi hili lielewe kabisa kabisa kuhusu mabadiliko mbalimbali ya sheria na miongozo inayotolewa ili itusaidie kwenye kutekeleza majukumu yetu, ni kundi muhimu sana kwenye mafunzo haya na ni imani yangu sote tumefanikiwa kushiriki wajumbe wote kwahiyo tutakapotoka tutakuwa na uelewa wa pamoja wa kuhusu kwamba tunasaidia watu wetu katika kujiongoza.” Amesema Ngoma.
Miongomi mwa wajumbe wa kamati ya usalama waliokuwepo kwenye mafunzo hayo, yanayohusisha pia watendaji wa kata na wakuu wa idara na vitengo wa halmashauri, ni pamoja na Mrakibu Mwandamizi wa Magereza Benjamin Kabisa, Mkuu wa Magereza wilaya ya Ruangwa, amesema “tumeona na kujifunza umuhimu wa haki, jinsi ambavyo tunapaswa kusimamia na kuzihifadhi lakini pia kulinda haki za binadamu, lakini pia kujua wajibu na majukumu yetu katika kazi zetu za kila siku.”
Wakili wa serikali Mkuu kutoka wizara ya Katiba na Sheria Bi. Joyce Mushi, ambaye ndio mratibu wa mafunzo hayo, amesema miongoni mwa mada zinazofundishwa ambazo zinawagusa moja kwa moja wajumbe wa kamati za usalama, ni Ulinzi na Usalama wa Nchi, inayofundishwa na mkufunzi kutoka Jeshi la Polisi Tanzania Kamishna Msaidizi wa Polisi Elisante Ulomi.
“Itawasaidia wao katika kuendelea kutatua migogoro na malalamiko kwa wananchi kwasababu wao kama vyombo vya usalama tunajua ni jukumu lao kuhakikisha eneo wanaloliongoza linakuwa salama..” Amesema Bi. Joyce.
Washiriki 42 wamepatiwa mafunzo hayo wilayani Ruangwa.