*************************
NA EMMANUEL MBATILO
Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa( TAKUKURU) imefanikiwa kuokoa kiasi cha shilingi bilioni 4 na kurejeshwa kwa wakulima na vyama vya Ushirika.
Akizungumza na wanahabari katika ofisi za makao makuu TAKUKURU, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa taasisi hiyo , Brig.Jen.John Mbungo amesema kuwa TAKUKURU imefanikiwa kuokoa kiasi hicho ambacho baadhi zimerejeshwa kwa wakulima na vyama vya Ushirika ama kutunzwa katika akaunti maalumu zilizofunguliwa kwa ushauri wa warajisi wa vyama vya ushirika na wakuu wa mikoa na wilaya kwa ajili ya kuzirejesha kwenye vyama vya ushirika ama wakulima.
“Taarifa iliyokabidhiwa TAKUKURU jumla ya fedha ambayo ilikuwa na viashiria vya ubadilifu wa fedha na mali pamoja na rushwa ni zaidi ya shilingi bilioni 124.Hata hivyo uchunguzi wa awamu ya kwanza uliofanywa na TAKUKURU mpaka sasa umefanikiwa kuchunguza kiasi cha shilingi bilioni 51 (51,794,221,683.09), wakati uchunguzi wa bilioni 72,259,029,190.91 unaendelea”. Amesema Brig.Jen.Mbungo.
Aidha, Brig.Jen.Mbungo amesema kuwa taasisi hiyo imeendelea kuboresha miundombinu ya kuwawezesha wananchi kuwasiliana nao na kuwapatia taarifa ambapo pamoja na kuwa na namba za simu ya dharura 113 ambayo ni bure na vilevile TAKUKURU imeanzisha TAKUKURU APPLICATION ambayo inamwezesha mwananchi kuwasilisha taarifa za wanaojihusisha na rushwa kupitia simu ya kiganjani.