Mkazi wa Mtaa wa Nera, Nyamagana akipiga kura leo.
Mkazi a Uhuru, Samiati Yahya,leo akipiga kura katika kituo cha Ghandhi Hall,
Mohamed Abdallah, akizungumza na waandishi wa habari bada ya kupiga kura leo.
Samiati Yahya , leo akihojiwa na waandishi wa habari baada ya kupiga kura.
Katibu wa BAKWATA Wilaya ya Nyamagana, akitoa maoni yake kwa waandishi wa habari, leo baada ya kupiga kura.
Msimamizi wa Uchaguzi Jiji la Mwanza, Akili Kiomoni Kibamba akizungumzia hali ya uchaguzi ulivyofanyika kwa amani na utulivu jijini humu leo.
…….
NA BALTAZAR MASHAKA, MWANZA
UCHAGUZI wa Serikali za Mitaa 2024,jijini Mwanza umefanyika leo kwa amani na utulivu, licha ya changamoto za mvua na matukio machache ya kiusalama.
Uchaguzi huo, ulilenga kuchagua viongozi wa mitaa na wajumbe, na ulivutia wananchi wengi ambao walijitokeza kwa wingi kutimiza haki yao ya kupiga kura.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Willbrod Mutafungwa, amethibitisha kuwa watu wanne wa CHADEMA wamekamatwa kwa tuhuma za kupora karatasi za kupigia kura na kufanya fujo.
Miongoni mwao yumo mgombea wa CHADEMA wa nafasi ya mwenyekiti wa mtaa wa Maliza,Athanas Kadaso pamoja na mawakala wa chama hicho katika vituo vya Lwanhima A, Ally Hussein na Edwin Otieno, wakala katika kituo cha Lwanhima B,anayedaiwa kukimbia na boksi la karatasi za kupigia kura.
Polisi wamewakamata watu hao wakiwa na karatasi 181 za kupigia kura ambazo hazikuwa zimetumika huku pia,wamemtia mbaroni Katibu wa CHADEMA ngazi ya wilaya,Amos Boniphace Ntobi,akidaiwa kufanya fujo na kuwazuia watu wasiende kupiga kura katika kituo cha Kabangwe,Mabatini kuwa hakipo katIka orodha ya vituo.
Vituo vya kupigia kura vilikuwa 1,000, na zaidi ya 406,000 ya wananchi walijiandikisha kupiga kura katika mitaa 175 ya Jiji la Mwanza, hata hivyo,viongozi wa CHADEMA wamejitokeza wakilazimisha wagombea wao kuwa mawakala kinyume na kanuni za uchaguzi huo.
Wakili Kiomoni Kibamba, msimamizi wa uchaguzi wa Jiji la Mwanza, ameeleza kuwa uchaguzi ulifanyika kwa amani, na kwamba mawakala kutoka vyama mbalimbali walishiriki kwa ufanisi.
Alisisitiza kuwa uchaguzi ulikuwa na ufanisi mkubwa na umekamilika kwa asilimia 99, huku wakikubaliana na dira ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha ushiriki wa wananchi katika uchaguzi kwa haki na amani kwa kuzingtia 4R.
Naye Msimamizi wa uchaguzi wa Ilemela,Wayayu amesema katika jimbo hilo hali ni shwari, hakuna changamoto kuhusiana na uchaguzi licha ya mvua kunyesha maeneo mbalimbali bado wananchi wameitikia na kujitokeza kupiga kura kwa amani, haki na uhuru.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda, amesisitiza kuwa matokeo ya uchaguzi yatatangazwa na msimamizi wa uchaguzi, na kwamba demokrasia itaheshimiwa kwa kutangaza mshindi kwa njia ya haki.
Katibu wa BAKWATA Wilaya ya Nyamagana, Sheikh Othman Masasi amikiri uchaguzi kufanyika kwa uhuru,amani na utulivu, huku akiwataka wananchi kusubiri matokeo wakia nyumbani.
Baadhi ya wananchi Samiati Yahya, Momahed Said na Omar Said, wamesema kuwa upigaji kura umefanyika kwa uhuru,haki,utulivu na amani,hivyo kuwawezesha wananchi kutumia haki yao ya kikatiba kuwachagua viongozi wanaowataka.
“Upigaji kura zoezi limekwenda vizuri, hakuna changamoto wala matukio ya kuzua hofu na taharuki,zaidi ya changamoto ya mvua iliyonyesha tangu asubuhi lakini baada ya kukatika watu wameongezeka,”amesema Samiati.