Na Sophia Kingimali.
SERIKALI imetoa rai kwa wawekezaji kuja kuwekezaji nchini kwani nchi ina rasilimali madini ya kutosha na imeweka mazingira mazuri ya uwekezaji katika sekta hiyo.
Akizungumza leo Novemba 21,2024 wakati akifunga mkutano wa kimataifa wa uwekezaji katika sekta ya madini akimuwakilisha Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanziba Dkt Hussein Alli Mwinyi Naibu spika wa bunge SMZ Mgeni Hassan Juma amesema lengo la serikali ni kuhakikisha madini yote yanaongezewa thamani hapa nchini kabla ya kusafirishwa kwenda nje ya nchi.
Amesema uwepo wa mkutano huo wanatarajia kupata maoni na ushauri mbalimbali kutoka kwa wadau jinsi ya kuboresha sekta hiyo.
“Rais Dkt Samia ameonyesha nia yake ya dhati ya kushirikiana na wawekezaji katika kukuza sekta ya madini nchi ili iweze kuleta manufaa kwa maendeleo ya Taifa”,Amesema.
Amesema serikali itahakikisha inajenga viwanda vingi nchini kwani itasaidia pia kuongeza ajira kwa vijana lakini pia kuyapa ubora madini yanayopatikana nchini.
Aidha ametoa rai kwa wachimbaji wadogo kutumia fursa zinazopatikana katika kuboresha shughuli zao za uchimbaji.
“Sekta ya uchimbaji mdogo imeimarishwa lakini pia nimejulishwa STAMICO na GST zimeendelea kutoa mitambo kwa wachimbaji wadogo hivyo nitoe rai kwa wachimbaji hawa kutumia fursa hiyo”,Amesema.
Kwa upande wake waziri wa madini Anthony Mavunde amesema kutokana na mwitikio mkubwa wa washiriki katika mkutano huo wanafikiria kuwa na eneo maalum kwa ajili ya mikutano ya sekta ya madini kama ilivyo kwa Maning Indaba kule south Afrika.
“Niwaombe wakuu wa mikoa katika maeneo yao kutenga maeneo maalum kwa ajili ya mikutano ya madini”,Amesema Mavunde.
Naye,Waziri wa maji,Nishati na Madini Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Shaibu Hassan Kaduara amesema Serikali ya Jamuhuri ya Muungano na Serikali ya mapinduzi Zanzibar zinashirikiana katika eneo la utafiti wa madini kwa manufaa ya pande zote.
“Hivi karibuni tulizindua ripoti ya utafiti wa madini visiwani Zanzibar tunaamini ushirikiano huu utasaidia pande zote za muungano ni fahari kubwa kwetu kujua kwamba tuna rasilimali hizi na tunaahidi kuzisimamia kwa manufaa ya vizazi vyetu”,Amesema Kaduara.
Akizungumzia kauli mbiu ya mkutano huo Naibu waziri wizara ya madini Dkt Steven kiruswa amesema kauli hiyo inakwenda sambamba na sera ya madini kuhusu oengezaji thamani madini kwani sera hiyo inataka madini yote yanayopatikana nchini yanapaswa kuongezewa thamani kabla ya kusafirishwa nje ya nchi ili kuongeza fursa ya ajira katika mnyororo mzima wa thamani katika madini.