Naibu Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Temeke Bw. Ismail Bukuku (kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na Katibu wa Chama cha Madereva na Wamiliki wa Pikipiki (CMPD) Wilaya ya Temeke Bw. Judica Pallangyo baada ya kuzindua kampeni ya kutoa elimu kwa jamii kuhusu kuzuia vitendo vya rushwa katika uchaguzi Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 27 mwaka huu, uzinduzi wa kampeni hiyo umefanyika leo Novemba 21, 2024 katika Ofisi za TAKUKURU Temeke, Dar es Salaam (PICHA NA NOEL RUKANUGA)
Naibu Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Temeke Bw. Ismail Bukuku akizungumza na waandishi wa habari leo Novemba 21, 2024 jijini Dar es Salaam kuhusu kampeni ya kutoa elimu kwa jamii ya kuzuia vitendo vya rushwa katika uchaguzi Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 27 mwaka huu kupitia Maafisa wa Usafirishaji Wilaya ya Temeke.
Naibu Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Temeke Bw. Ismail Bukuku akiwa katika picha ya pamoja na Maafisa Usafirishaji Wilaya ya Temeke.
………….
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Temeke kwa kushirikiana na Maafisa Usafirishaji Manispaa ya Temeke wamezindua kampeni ya kutoa elimu kwa jamii kuhusu kuzuia vitendo vya rushwa katika uchaguzi Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 27 mwaka huu.
Kampeni hiyo inatoa fursa wa maafisa wa usafirishaji wakiwemo madereva wa bajaji kubandika ujumbe katika usafiri huo ambao umelenga kuhamasisha jamii kuacha kushiriki vitendo vya rushwa katika uchaguzi wa serikali za mitaa.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Novemba 21, 2024 jijini Dar es Salaam, Naibu Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Temeke Bw. Ismail Bukuku, amesema kuwa wanaamini maafisa usafirishaji watapeleka ujumbe kwa wananchi kwa haraka kwani ni wadau wakubwa katika mapambana dhidi ya rushwa.
Bw. Bukuku amesema kuwa lengo ni kuhakikisha wanaamini wananchi wanatumia fursa yao vizuri ya kwenda kuchagua viongozi au kuchaguliwa kujihusisha na vitendo vya rushwa.
“Lengo kuu ni kuzuia rushwa katika chaguzi za kisiasa, kuzuia rushwa ni jukumu lako na langu, tukatimize uwajibu wetu” amesema Bw. Bukuku.
Katibu wa Chama cha Madereva na Wamiliki wa Pikipiki (CMPD) Wilaya ya Temeke Bw. Judica Pallangyo, ameishukuru takukuru kwa kuwashirikisha katika zoezi la kuzuia vitendo vya rushwa.
Amesema kuwa madereva wa pikipiki na bajaji wanafanya kazi kwa ushirikiano hivyo wataendelea kutoa elimu ambayo wameipata hasa kipindi hiki cha uchaguzi wa Serikali za mitaa.
“Tutaendelea kutoa elimu kwa jamii hadi uchaguzi mkuu ili kuhakikisha tunatimiza malengo yetu ya kumuunga mkono Rais Dkt. Samia Suruhu Hassani kupinga vitendo vya uhalifu ikiwemo kutoa rushwa” amesema Bw. Pallangyo.
Maafisa Usafirishaji katika usafiri wao watakuwa wamebeba ujumbe ambao unasomeka : Kuzuia rushwa ni jukumu langu na lako, tutimize uwajibu wetu “Tumia vyema fursa ya kuchagua au kuchaguliwa bila vitendo vya rushwa”.