*Amtaka Mkandarasi barabara ya Utete-Kingupira kuwasilisha mpango kazi wake
Rufiji, Pwani
Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Mhandisi Victor Seff amemtaka Mkandarasi MAC Contractor Ltd anayejenga Daraja la Mohoro lililopo Wilayani Rufiji Mkoa wa Pwani kukamilisha ujenzi wa nguzo mbili zilizobakia kwenye ujenzi wa daraja hilo kabla ya msimu wa mvua kuanza.
Mhandisi Seff ametoa agizo hilo ikiwa ni siku tatu tangu kupita eneo hilo la ujenzi na leo kurudi tena ili kujionea hatua ya kuangalia maagizo yake ya awali aliyoyatoa kama yametekelezwa.
Aidha, Mhandisi Seff, amemtaka Mhandisi Mshauri wa TREECO Mhandisi Emmanuel Mahimbo kumsimamia Mkandarasi MAC ili amalize kazi kwa wakati.
Katika hatua nyingine Mhandisi Seff ametembelea tena mradi wa ujenzi wa barabara ya Utete-Kingupira (Km. 32) inayojengwa kwa kiwango cha changarawe kwa kutumia Teknolojia Mbadala ya ECOROADS na Mkandarasi NRST LIMITED CIVIL WORKS CONTRACTOR JV DASHAS COMPANY LIMITED.
Mhandisi Seff hakuridhishwa na kasi ya utekelezaji wa mradi huo na kumuelekeza Kaimu Meneja wa TARURA Wilaya ya Rufiji Mhandisi Nicolaus Ludigery kuhakikisha Mkandarasi NRST anawasilisha mpango kazi wake unaoonyesha namna atakavyofidia siku zilizopotea na kukamilisha kazi kwa wakati, vinginevyo hatua za kimkataba zitachukuliwa.
Mradi wa ujenzi wa barabara ya Utete-Kingupira umepangwa kukamilika mwezi Aprili 2025.