Mratibu wa Taifa wa Mtandao wa kutetea haki za Binadamu, Onesmo Ole Ngurumwa  akizungumza na waandishi wa habari mkoani Arusha
Mtendaji  Mkuu  wa  (TPSF),  Raphael Maganga akizungumza na waandishi wa habari mkoani Arusha
……..
Happy Lazaro,Arusha.

MTANDAO wa Watetezi wa haki za binadamu Tanzania umeazimia  kukutana na Rais Samia Suluhu Hassan kwa ajili ya kuzungumzia hatma ya masuala ya utekaji na ukatili  yanayoendelea nchini pamoja na kumkumbusha mikataba ya kimataifa ya kupinga ukiukwaji wa haki za binadàmu.

Akizungumza na waandishi wa habari katika mkutano mkuu wa 13 wa wanachama wa mtandao  THRDC unaoendelea katika wiki ya AZAKI jijini Arusha,Mratibu wa Taifa wa Mtandao wa kutetea haki za Binadamu, Onesmo Ole Ngurumwa amesema mkutano huo umelenga  kuangazia masuala mbalimbali ikiwemo kupitia na kuidhinisha taarifa ya nusu muhula ya hali ya haki za binadamu ,utekelezaji wa mapendekezo ya kipindi kilichopita.
Tumekutana hapa kwa ajili ya kupitia na kuidhinisha taarifa ya nusu muhula kuhusu hali ya haki za binadamu katika  kuangalia utekelezaji wa  mapendekezo,pamoja na kuketi na wafanyabiashara wenye makampuni ya kibiashara Tanzania ambao wanaweza kutuunga mkono kupitia rasilimali fedha katika mapambano ya utetezi wa haki za binadamu kuhusu ukatili”Ole Ngurumwa. 

Amesema wadau wa haki za binadamu wamekuwa na changamoto kubwa katika kupambana na utekaji, mauaji na ukiukwaji wa haki za binadamu na hivyo wameomba kukutana na Rais Samia ili kuona namna ya kupata suluhu ya kukabiliana na changamoto hizo zinazogharimu maisha ya watu.

“Tulitoa mapendekezo yetu kwa Rais Samia kuhusu uundaji wa tume rasmi ya kiraia ya kudumu inayohusisha watu wengi na tulimshauri aridhie mikataba miwili ya kimataifa  inayopinga masuala ya utekaji na ukatili na ndio maana leo tumeadhimia kwenda kukutana naye  baada ya miaka mitatu kupita “

Amesema mkutano huo wenye ajenda ya Kuboresha namna ya kupata Rasilimali za ndani,unalenga kumshawishi Rais aridhie kusaini mikataba miwili ya kimataifa inayopinga masuala ya ukatili nchini.

Mtendaji  Mkuu  wa  (TPSF),  Raphael Maganga ambaye alikuwa mgenirasmi  amesema jukumu kubwa la sekta binafsi ni kuona namna inayoweza kushirikiana na taasisi mbalimbali kukuza utetezi wao katika haki za binadamu.

Maganga amesisitiza kuwa sekta binafsi zina wajibu wa kutetea haki za binadamu kama watoto,vijana na wanawake katika nyanja mbalimbali ikiwemo elimu ili kuwawezesha kufanya kazi zao kwa uhuru na ufanisi zaidi.

Amesema taasisi za kutetea haki za binadamu zimefanikiwa kwa kiasi kikubwa ila zinapaswa kuwa imara na kufanya kazi zao kwa ufanisi zaidi ili kuhakikisha jamii yote inakuwa na haki sawa.