Meneja Mkuu wa Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO) Haji Haji akitoa maelezo mafupi ya kumkaribisha Waziri wa Maji Nishati na Madini Mhe,Shaibu Hassan Kaduara katika Mkutano na Wafanyakazi wa Shirika la Umeme (ZECO)Saateni Zanzibar.
NA SABIHA KHAMIS – MAELEZO
Waziri wa Maji, Nishati na Madini Zanzibar Mhe. Shaib Hassan Kaduara amewataka wafanyakazi wa Shirika la Umeme Zanzibar kuzingatia taratibu na msingi bora ya kufanyakazi ili kuweza kufanyakazi kwa umakini na uwadilifu.
Akizungumza na wafanyakazi wa Shirika hilo katika uwanja wa Ofisi hizo Saateni, Wilaya ya Mjini Unguja amesema ushirikiano ndio nguzo muhimu katika utendaji wa kazi hivyo ni vyema kutii sheria, taratibu na kanuni za utumishi.
“Wacha sasa tufanyekazi kama inavyotuelekeza kwa ushirikiano uliokuwepo katika taratibu za kazi na kutii sheria za utumishi na kanuni zake ili kila mmoja akae kwenye mstari ambao anatakiwa akae” alisema Waziri Kaduara.
Aidha amesema kila anaekiuka kanuni na taratibu za kazi kuchukuliwa hatua madhubuti za kisheria pamoja na kulipa fidia kwa Shirika la Umeme, fedha ambazo zitasaidia kutimiza malengo ya Ofisi.
Ameeleza kuwa kwa yoyote asietaka kufuata utaratibu wa kazi akae nje ya kazi ili kupisha wenye ari na uhitaji wa kufanyakazi ili kuleta maendeleo katika nchi.
Hata hivyo amemuagiza Meneja wa Shirika hilo kumsimamisha kazi ndugu Nishani Juma na uchunguzi kuanza mara moja kufuatia kosa la kuunga umeme kinyume ya taratibu na kanuni za Shirika.
“Hatua hiyo haitoishia hapa kila anayehusika na kufanya ubadhirifu huo hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake na hadi sasa jumla ya watumishi 15 tunaanza kuwashughulikia kwa utaratibu na wengine watafuata” amesema Waziri.
Sambamba na hayo amewaagiza wafanyakazi wa Shirika hilo kutafuta mfumo utakao tumika kutuma maombi ya kuungiwa umeme moja kwa moja na kuacha kupanga foleni katika Ofisi ambazo hupelekea upotevu wa fedha za Serikali pamoja na rushwa kwa wafanyakazi.
Ameeleza kuwa kwa kila mwezi Bilioni 3.6 zinapotea kutokana na kukithiri kwa vitendo vya wizi katika shirika hilo ambavyo hupelekea kurudisha nyuma maendeleo ya Nchi.
Kwa upande wake Meneja Mkuu wa Shirika la Umeme Haji Haji amesema wameweza kutatua changamoto ya mtindo wa biashara kwa kuongeza wadau wengine wa mitandao ya Benki ikiwemo PBZ, CRDB, NMB, NBC na TTCL ambao utasaidia kuokoa fedha nyingi za shirika hilo.
Alifahamisha kwamba Vituo vilivyokuwa vinatumia kwa mauzo ya umeme vimefunga na kukodisha kwa wakala ambao ni wadau wa mauzo ya umeme , jambo ambalo limeleta tija kubwa ambapo kwa sasa kuna wastani wa mauzo ya shilingi Milioni 11 mpaka 12 kwa kila siku ambapo hapo nyuma vituo hivyo vilikuwa vinauza wastani wa shilingi milioni 1.2 kwa siku.
Amefafanua kuwa kwa kipindi cha muda mfupi wamepata mafanikio makubwa kwa kuunganisha nyaya za umeme kuelekea Tumbatu ambazo zilikuwa zimekatika kwa miaka miwili iliyopita na kusababisha Kisiwa cha Tumbatu kukosa umme wa uhakika kutokana na miundombinu kutofanya kazi vizuri.