Na Sophia Kingimali
Aliyekuwa mgombea wa nafasi ya uwenyekiti wa Chama cha Alliance for Democratic Change (ADC), Doyo Hassan Doyo amekata rufaa kwenye kamati ya rufaa ya chama hicho, kupinga uchaguzi uliofanyika baada ya kutoridhika na matokeo,lakini pia ameituhumu kamati ya uchaguzi pamoja na mwenyekiti aliyemaliza muda wake Hamad Rashid Mohamed, kwa kukiuka katiba na kanuni za chama hicho.
Akizungumza na wanahabari leo Julai Mosi 2024, Doyo amesema amekata rufaa kwa mujibu wa kanuni za chama za mwaka 2019 kanuni ndogo ya tatu, inayozungumia haki ya rufaa ambayo itatolewa kwa mgombea tu.
“Sheria hii inamtaka atakayekata rufaa kuwasilisha kusudio ndani ya saa 24, baada ya uchaguzi na baadaye rufaa yenyewe ambayo yote tumeshayafanya,”amesema Doyo.
Msingi wa rufaa
Kwa mujibu wa Doyo amesema sababu ya kukata rufaa ni pamoja mkutano wa uchaguzi kuongozwa na mwenyekiti anayemaliza muda wake Hamad Rashid Mohamed badala ya wajumbe kumchagua mwenyekiti wa muda.
Sababu nyingine ni mwenyekiti wa muda baada ya kupatikana ataendesha shughuli ya kumpata mwenyekiti wa kudumu na baada ya hapo, atamkabidhi kiti kwaajili ya uchaguzi wa makamu mwenyekiti Bara na Zanzibar.
“Hapa katiba ilivunjwa mwenyekiti anayemaliza muda wake aliongoza kikao kile kinyume na katiba, na hata alipopatikana hakumkabidhi kiti kuendelea na majukumu yake,”amesema Doyo.
Aidha Doyo amesema sababu nyingine ni msimamizi wa kutowapa nafasi wapigakura nafasi kinyume na kifungu n kwa kuwasimamia, na kuwaelekeza nani wakumpigia kura.
“Tunapiga matokeo yote ya uchaguzi pamoja na uendeshaji wake na utangazaji wa matokeo, mambo yote haya yalifanyika mbele ya Msajili Msaidizi wa Vyama vya Siasa,”amesema.
Nao baadhi ya wanachama wa chama hiko wamesema hawakuridhishwa na kilichofanywa na mwenyekiti aliyemaliza muda wake hivyo wataungana na Doyo kuhakikisha haki inapatatika.
Lakini pia baadhi yao waliopewa nafasi ya uongozi katika maeneo mbalimbali ndani ya chama wamezikataa nafasi hizo mpaka pale haki yao itakapopatikana.
Juni 29 mwaka huu chama hicho kilifanya uchaguzi mkuu wa nne ambapo baadhi, ya viongozi wamemaliza muda wao wa kipindi cha miaka kumi, kwa mujibu wa katiba akiwemo aliyekuwa mwenyekiti Hamad Rashid Mohamed.