Mjumbe wa Kamati Kuu ya Taifa ya Chama cha ACT WAZALENDO, Dkt. Nassra Nassor Omar, amewahimiza viongozi wa majimbo kuhakikisha wanafanya vikao vya chama kwa mujibu wa Katiba, akisisitiza kuwa uhai wa chama unategemea utekelezaji wa vikao hivyo.
Dkt. Nassra, ambaye pia ni Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi kupitia nafasi za viti maalum kwa tiketi ya chama hicho, aliyasema hayo jioni ya leo, tarehe 14 Juni 2026, wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Kikatiba wa Jimbo Jang’ombe
Alisema chama kisichokuwa na vikao vya mara kwa mara hakiwezi kuonekana kuwa kina uhai, kwani vikao ndiyo msingi wa uendeshaji na uimara wa chama.
“Kwa hiyo, Mkutano Mkuu mliofanya leo unaonesha ni kwa kiasi gani ACT WAZALENDO kipo imara kuanzia ngazi ya Taifa hadi matawini,” alisema Dkt. Nassra.
Aidha, alieleza kuwa mafanikio ya chama yanategemea mshikamano wa viongozi na wanachama, na kuwataka viongozi wa Jimbo la Jang’ombe kuendelea kushirikiana kwa karibu na wanachama wao.
“Umoja ndiyo nguvu yetu, na nawaombeni sana tuudumishe umoja wetu,” alisisitiza Dkt. Nassra.
Kwa upande wake, Katibu wa Jimbo la Jang’ombe, Ali Miraji, akisoma taarifa ya mwaka ya jimbo, alisema Mkutano Mkuu huo ulitimiza akidi kwa kuhudhuriwa na wajumbe 47 kati ya wajumbe 65 wenye haki ya kushiriki mkutano huo.
Tayari hadi sasa majimbo 22 kati ya majimbo 50 ya chama hicho Unguja na Pemba tayari yamefanya mikutano yao ya kikatiba.

