*******************************************
Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe. Paul Makonda leo ametembelewa ofisini kwake na Pascal Cassian ambae amefika kwa lengo la kutoa shukrani na kumthibitishia kuwa Amepona tatizo la Mfumo wa Figo na Kibafu cha mkojo lililokuwa likimsumbua kwa muda mrefu na kumfanya familia yake kupoteza matumaini.
Itakumbukwa RC Makonda aliona taarifa ya tabu na Mateso aliyokuwa akiyapata Pascal Cassian kupitia mitandao ya kijamii na kuagiza atolewe nyumbani apelekwe Hospital ya Muhimbili ambapo alitoa ahadi ya kugharamia matibabu yake ndani na nje ya nchi na hivi karibuni alimpatia kitita cha fedha kwaajili ya Matibabu nchini India, Tiket ya Ndege kwa watu watatu waliomsindikiza pamoja na fedha ya malazi kwa siku zote walizokuwa wakipata matibabu Nchini India.
RC Makonda amemshukuru Mungu kwa kutenda miujiza kwa Pascal ambae aliondoka nchini akiwa amebebwa huku akiwa na mifuko ya kuhifadhi haja ndogo na leo Pascal anamtembelea RC Makonda ofisini akiwa anatembea kwa miguu na akiwa anajisaidia haja ndogo kama alivyokuwa zamani.
Aidha RC Makonda amemshukuru Mungu kwa kumponya mtu ambae baadhi ya watu walisema hawezi kupona na wengine kusema hadharani kuwa pesa alizotoa RC Makonda kwaajili ya matibabu ni sawa na kutupa pesa kwenye shimo la choo.
RC Makonda amewashukuru watu wote waliomuunga mkono kwa kumuombea Pascal hadi ameweza kupona huku akiwataka watanzania kuwa na moyo wa upendo na kusaidiana.
Kwa upande wake Pascal Cassian amemshukuru RC Makonda na kumuhakikishia kuwa amepona na sasa anaweza kuendelea na shughuli zake za kutafuta kipato kama alivyokuwa awali.
Nae Mke wa Pascal Cassian na watoto wake wamesema kuwa awali hao na familia pia walikata tamaa kwa hali aliyokuwanayo Pascal lakini walipata tumaini jipya pale walipohakikishiwa na RC Makonda atasimama bega kwa bega na familia hadi kuhakikisha anapona.