Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, mhandisi Zephania Chaula (wapili kushoto) akipakua chakula kilichoandaliwa na mdau wa maendeleo Charlea Manyalu (watatu kulia) kwa ajili ya watoto yatima wa mji mdogo wa Mirerani.

Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro mhandisi Zephania Chaula akizungumza na mmoja kati ya watoto waliohudhuria tafrija iliyoandaliwa na mdau wa maendeleo Charles Mnyalu kwa ajili ya watoto yatima, ambapo aliwaandalia chakula na kuwagawia madaftari, kalamu na nguo.

Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro mhandisi Zephania Chaula akiwa kwenye picha ya pamoja na watoto yatima wa mji mdogo wa Mirerani katika tafrija iliyoandaliwa na mdau wa maendeleo Charles Mnyalu.
************************************
|
DC SIMANJIRO AITAKA JAMII IMUIGE MNYALU
MKUU wa Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, mhandisi Zephania Chaula ameitaka jamii kuiga mfano wa mdau wa maendeleo Charles Mnyalu kwa kuwajali yatima ambao ni viongozi wa miaka ijayo kwani jukumu hilo siyo la serikali peke yake.
Mhandisi Chaula aliyasema hayo mji mdogo wa Mirerani kwenye chakula cha pamoja kwa yatima kilichoandaliwa na mdau wa maendeleo Charles Mnyalu, aliyewagawia kalamu, madaftari na nguo.
Alisema jamii iige mfano wa Mnyalu ambaye amejitolea kuwasaidia watoto hao bila ubaguzi wowote ule kwani nao watajihisi faraja na kusoma kwa bidii ili miaka ijayo wawe viongozi wakubwa kwenye nchini hii.
Alisema watoto yatima wanapaswa kusaidiwa kwa hali na mali kwani wengi wao wazazi wao wamefariki dunia hivyo watu wengine kama Mnyalu wanatakiwa kuliangalia hilo kwa jicho la kipekee.
“Watoto yatima hawa ni wa kwetu ndiyo viongozi wa leo na kesho tusipowatunza sasa hatutakuwa na viongozi wazuri miaka ijayo, kila mmoja kwa namna anavyoweza aige alivyofanya Mnyalu,” alisema mhandisi Chaula.
Hata hivyo, mdau huyo wa maendeleo, Charles Mnyalu alisema ameamua kujitolea kidogo alichojaaliwa ili kuwapa faraja watoto hao yatima.
Alisema japokuwa yeye hana utajiri wa kutosha ameona ajitolee kidogo alichonacho kwani maandiko ya madhehebu ya Kikristo yanaagiza ukiwa na mashati mawili mgawie mwenzako moja.
“Watoto wadogo nawapenda sana tuombe Mungu tutakutana tena kwenye sherehe za Christmas mwezi Desemba ninawatakia kila la heri ndugu zangu wapendwa,” alisema Mnyalu.
Mmoja kati ya watoto wa eneo hilo, Hamis Ramadhan alimshukuru mdau huyo wa maendeleo Mnyalu kwa kujitolea kuwasaidia watoto hao yatima.
“Japokuwa hatuna wazazi lakini kitendo cha kufurahi pamoja na sisi tukale, tukanunuliwa nguo, madaftari na kalamu tumepata faraja kubwa,” alisema Ramadhan.