Mkuu wa Polisi Wilaya ya Ileje Mrakibu wa Polisi (SP) Manda Rugoma amewaomba viongozi wa dini na wazee wa kimila wilayani humo kushirikiana na Jeshi la Polisi katika suala la malezi na maadili katika maeneo yao ili jamii iondokane na changamoto ya uhalifu.
Mrakibu Rugoma amesisitiza hayo Juni 12, 2024 na kusema kuwa endapo kila kiongozi akisimamia kikamilifu katika suala la maadili basi jamii itaondokana na mmomonyoko wa maadili na uhalifu utapungua katika maeneo yetu.
Vilevile amewataka viongozi hao kutoa elimu kwa wazazi na walezi juu ya malezi bora kwa watoto wao ikiwa ni pamoja na kuwalea katika misingi ya dini ili wachukie na kukemea matendo maovu.
Sambamba na hayo aliwaomba viongozi hao kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu ili zishughulikiwe kwa haraka ili jamii iendelee kuwa salama.