Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete, amewasihi watumishi wa umma kuhamishia ari, nidhamu na mshikamano walioonesha katika michezo kwenye maeneo yao ya kazi ili kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wananchi.
Mhe. Kikwete ametoa rai hiyo Tarehe 7 Oktoba, 2026 wakati akifunga Mashindano ya 40 ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali Tanzania (SHIMIWI) yaliyofanyika mkoani Kilimanjaro, akisisitiza kuwa michezo ina nafasi muhimu katika kuimarisha afya ya mwili na akili ya watumishi na kuwajengea utayari wa kutekeleza majukumu yao.
Amesema mashindano hayo yamewakutanisha zaidi ya wanamichezo 3,400 kutoka taasisi mbalimbali za Serikali na kutoa fursa ya kujenga mahusiano, kuimarisha ushirikiano na kushiriki shughuli za kijamii.
Katika hatua nyingine, Mhe. Kikwete amewapongeza washiriki kwa kuchangia zaidi ya Shilingi milioni 24 kwa ajili ya kusaidia makundi yenye uhitaji, ikiwemo watoto wenye mahitaji maalumu na wanaopatiwa matibabu ya saratani katika Hospitali ya KCMC.
Ameipongeza pia Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Kamati ya Utendaji ya SHIMIWI pamoja na wadau mbalimbali kwa kufanikisha mashindano hayo, huku akitaka changamoto zilizojitokeza mwaka huu kufanyiwa kazi ili kuongeza ubora wa mashindano yajayo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa SHIMIWI, Daniel Mwalusamba, amewataka waajiri kuendelea kutoa nafasi kwa watumishi kushiriki michezo na kuimarisha utamaduni wa kufanya mazoezi mahali pa kazi.
Mwalusamba amesema pamoja na kuimarisha afya, michezo inapaswa kuwa chachu ya nidhamu, uwajibikaji na kuongeza ufanisi wa watumishi katika kutekeleza majukumu yao.
Mashindano hayo yamehitimishwa huku ikielezwa kuwa SHIMIWI 2027 inatarajiwa kufanyika mkoani Arusha, baada ya Kilimanjaro kuwa mwenyeji wa mashindano hayo ya mwaka huu.

