Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Sixtus Mapunda, amelipongeza Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Temeke kwa juhudi za kuimarisha utoaji wa huduma ya umeme kwa ufanisi, ikiwemo kushughulikia changamoto za dharura kwa wakati.

Aidha, amelitaka Baraza la Madiwani la Manispaa hiyo kushirikiana na TANESCO katika kuwafikia wananchi na kutatua changamoto za huduma ya umeme, kwani nishati ni kichocheo muhimu cha maendeleo ya Taifa.

Akizungumza leo Oktoba 7, 2026, wakati akifungua kikao cha wadau wa nishati ya umeme Mkoa wa Temeke kilichofanyika katika Ukumbi wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Kurasini, Dar es Salaam, Mapunda amezitaka taasisi nyingine wilayani humo kuiga mfano wa TANESCO kwa kutekeleza majukumu yao kwa kujituma zaidi, hatua inayosaidia kuongeza ufanisi .

“TANESCO Mkoa wa Temeke wako mbele katika utambuzi wa utoaji wa huduma kwa jamii. Wafanyakazi wao wanajituma, ni wazalendo na wanafahamu wanachokifanya,” amesema Mapunda.

Kwa upande wake, Meneja wa TANESCO Mkoa wa Temeke, Mhandisi Nickson Babu, amesema shirika limeweka mipango na mikakati mbalimbali ya kuboresha huduma, ikiwemo kuimarisha mawasiliano na wateja kupitia njia mbalimbali, pamoja na kupiga namba ya bure 180, ili kuwawezesha kupata msaada kwa urahisi wanapokumbana na changamoto.

“Pia tumejipanga kumuunganishia mteja umeme ndani ya muda mfupi kulingana na mahitaji yake, pamoja na kuendelea kuboresha miundombinu iliyobainika kuwa na dalili za uchakavu, ili kuhakikisha huduma inakidhi mahitaji ya wateja,” amesema Mhandisi Babu.

Kwa upande wao wadau wa nishati ya umeme Mkoa wa Temeke akiwemo
Mkuu wa Mahusiano Kamal Group, Bi. Emma Mwenda, wamefurahishwa na mipango ya TANESCO ya kuimarisha huduma, huku wakisisitiza umuhimu wa nishati ya umeme katika kuendesha shughuli za uzalishaji na biashara.

Kikao hicho kilihudhuriwa na wadau mbalimbali, wakiwemo Wabunge, Madiwani wakiongozwa na Mstahiki Meya wa Manispaa ya Temeke, Mhe. Uzairu Athuman, pamoja na wateja wakubwa waliotunukiwa zawadi kama ishara ya kutambua mchango wao.

Pia Kikao hicho ni sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya Huduma kwa Wateja 2026, inayoongozwa na kaulimbiu “Mbele Zaidi Kihuduma.”