Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa leo Mei 14, 2024 amefungua Mashindano ya Klabu Bingwa Netiboli Afrika Mashariki katika uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar Es Salaam.
Akizungumza wakati wa ufunguzi huo Msigwa amewataka wadau wa mchezo huo kuendeleza jitihada za kukuza mchezo wa netiboli kutokana na umuhimu wake kwa jamii ikiwa ni pamoja na kuimarisha afya na kuleta ajira
“Mchezo wa netiboli una heshima kubwa kwa nchi yetu na Afrika naomba muendelee kuukuza, hapa katikati ulikua unalegalega, CHANETA hakikisheni mnafanya vizuri ili tufike tunapotaka” Amesisitiza Msigwa
Aidha, amesema Serikali itachangia kiasi cha shilingi milioni kumi ili kuongeza nguvu kwenye mashindano hayo yaliyoanza Mei 12, 2024 ambapo timu 12 kutoka nchi nne zinashiriki na yanatarajiwa kuhitimishwa Mei 18 mwaka huu.
Ufunguzi huo pia umehudhuriwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Suleiman Serera, Katibu Mtendaji wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Neema Msitha na Maafisa wengine wa Serikali.