Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip
Mpango akiwa na Makamu wa Pili wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhe.
Hemed Suleiman Abdulla pamoja na viongozi mbalimbali wakati wa Dua na
Maombi ya kuliombea Taifa kuelekea Miaka 60 ya Muungano yaliyofanyika
katika Uwanja wa Jamhuri mkoani Dodoma tarehe 22 Aprili 2024.
Viongozi pamoja na Wananchi mbalimbali wakishiriki Dua na Maombi ya
kuliombea Taifa kuelekea Miaka 60 ya Muungano yaliyofanyika katika Uwanja
wa Jamhuri mkoani Dodoma tarehe 22 Aprili 2024.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip
Mpango akihutubia wakati wa Dua na Maombi ya kuliombea Taifa kuelekea
Miaka 60 ya Muungano yaliyofanyika katika Uwanja wa Jamhuri mkoani
Dodoma tarehe 22 Aprili 2024.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip
Mpango akisalimiana na viongozi mbalimbali wa dini mara baada ya
kuhitimishwa kwa Dua na Maombi ya kuliombea Taifa kuelekea Miaka 60 ya
Muungano yaliyofanyika katika Uwanja wa Jamhuri mkoani Dodoma tarehe 22
Aprili 2024.
Viongozi mbalimbali wa dini walioshiriki katika Dua na Maombi ya kuliombea
Taifa kuelekea Miaka 60 ya Muungano yaliyofanyika katika Uwanja wa
Jamhuri mkoani Dodoma tarehe 22 Aprili 2024.
……………………….
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip
Mpango ameungana na viongozi wa dini pamoja na watanzania kwa ujumla
katika Dua na Maombi kwaajili ya kuliombea Taifa kuelekea Miaka 60 ya
Muungano, Dua na Maombi hayo yamefanyika katika Uwanja wa Jamhuri
mkoani Dodoma leo tarehe 22 Aprili 2024.
Akihutubia mara baada ya maombi na dua ya kuliombea Taifa, Makamu wa
Rais amesema Katika kipindi cha miaka 60 ya uwepo wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Taifa limeendelea kupiga hatua katika sekta
mbalimbali na hivyo kuendelea kuboresha maisha ya Watanzania.
Amesema tangu Muungano ulipoasisiwa mwaka 1964 umeendelea kuimarika
mwaka hadi mwaka ambapo changamoto mbalimbali za Muungano zimekuwa
zikitatuliwa kupitia mazungumzo ya pamoja na hivyo kujenga maelewano na
mshikamano katika Taifa. Amesema mafanikio hayo ni kutokana na udugu na
ushirikiano wa wananchi wa pande zote mbili za Muungano uliokuwepo tangu
zamani na nia ya dhati ya kujenga nchi na jamii inayozingatia misingi ya
uhuru, haki, udugu na amani. Amewasihi wananchi kuendelea kuenzi na
kudumisha tunu za Taifa ambazo ni amani, umoja, mshikamano, utu, haki,
heshima ya mwanadamu, uhuru na demokrasia.
Aidha Makamu wa Rais amesema wakati ikitimia miaka 60 ya Muungano,
bado ni muhimu kuendelea kufanya kazi kwa bidii ili kuongeza kasi ya
maendeleo, kukuza ustawi wa jamii na kutatua changamoto mbalimbali
zinazokabili Taifa. Halikadhalika amewasihi watanzania wote kwa pamoja kwa
kuongozwa na viongozi wa dini, Serikali, wazazi, walezi na walimu kuwajibika
kuendelea kukabiliana na mmomonyoko wa maadili katika Taifa unaopelekea
kuongezeka kwa matendo yanayokiuka mila na desturi za Kitanzania ikiwemo
uhalifu, ukatili, matumizi ya dawa za kulevya na mengineyo ambayo
hayampendezi Mwenyezi Mungu.
Katika hatua nyingine Makamu wa Rais amesema serikali itaendelea kuchukua
hatua katika kudhibiti uhalifu na ufujaji wa fedha za umma. Amewataka
wananchi kutoa taarifa kwa vyombo husika pale uovu unapofanyika katika
jamii ili hatua ziweze kuchukuliwa. Ametoa wito kwa Mihimili yote kufanya
kazi kwa ushirikiano kwa manufaa ya nchi na watu wake. Amewasihi
Watanzania kutumikia nchi kwa haki uadilifu na uzalendo.
Vilevile Makamu wa Rais amesema Serikali inatambua na kuthamini
ushirikiano mzuri uliopo baina yake na Taasisi za dini nchini na itaendeleza
ushirikiano huo kwa manufaa na ustawi wa Taifa. Amewashukuru viongozi
wote wa dini nchini kwa kuendelea kuliombea Taifa pamoja na kuendelea
kukemea maovu, kuonya, kufundisha maadili mema na kutoa huduma za
kiroho na kijamii kwa Watanzania. Aidha, amewapongeza Viongozi wa Dini
kwa mchango mkubwa katika kuhakikisha Watanzania wanaendelea kubaki
wamoja na kuendelea kushirikiana licha ya tofauti za dini, kabila, rangi, ufuasi
vyama vya siasa au mahali wanapotoka.
Kwa upande wake Makamu wa Pili wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhe.
Hemed Suleiman Abdulla amesema vijana wa sasa wana kisa sababu
kuhakikisha wanaulinda, kuusimamia, kuimarisha na kutetea muungano ili
uendelee kudumu daima na vizazi vijavyo viukute Muungano ukiwa salama na
wenye mafanikio makubwa.
Amesema Muungano unadumisha umoja, amani, mshikamano na upendo na
kutoa uhuru kwa wananchi wa pande zote mbili kuweza kufanya shughuli za
kijamii na kiuchumi.
Dua na Maombi hayo yameongozwa na viongozi wa dini pamoja na
kujumuisha waumini, waimbaji wa muziki wa dini wa kikristo na kiislamu.
Aidha maombi hayo yamehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali
akiwemo Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Juma, Waziri Nchi Ofisi ya
Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Dkt. Selemani Jafo, Waziri wa Nchi
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais (Sera Uratibu na Baraza la Wawakilishi)
Hamza Hassan Juma, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na
Uratibu) Jenista Mhagama, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule,
Wabunge pamoja wananchi mbalimbali.