Na Mwandishi wetu, Mirerani
MKURUGENZI mtendaji wa Mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira Arusha (AUWSA) mhandisi Idd Msuya amesema mradi wa maji mji mdogo wa Mirerani utakapokamilika utanufaisha watu 57,000 wa Tarafa ya Moipo wilayani Simanjiro mkoani Manyara.
Mhandisi Msuya ameeleza hayo kwenye ziara ya Mwenyekiti wa jumuiya ya Wazazi wa CCM Taifa Fadhili Rajab Maganya iliyofanyika mji mdogo wa Mirerani wilayani Simanjiro.
Mhandisi Msuya amesema mradi huo ukikamilika utanufaisha wakazi hao wa Tarafa ya Moipo wa kata nne za Mirerani, Endiamtu, Naisinyai na Shambarai.
Amesema mradi huo ukikamilika utatumia gharama za shilingi bilioni 4.3 na hadi sasa umetumia shilingi bilioni 2.5.
Mwenyekiti wa Wazazi wa CCM Taifa, Fadhili Rajab Maganya amewasihi AUWSA wakamilishe mradi huo kwa wakati ili jamii ya eneo hilo inufaike na maji hayo.
“Mhandisi Idd Msuya natambua utendaji kazi wako, nilipofika kwenye mradi sikufurahi ila nimepata faraja nimekuona hapa,” amesema.
Mwenyekiti wa Wazazi wa CCM Mkoa wa Manyara, Janes Darabe amesema mhandisi Msuya ameshafanya kazi BAWASA hivyo anatambua uwajibikaji wake mahiri hivyo anatarajia mradi huo kukamilika kwa wakati.
Mwenyekiti wa chama cha wachimbaji madini Mkoa wa Manyara, MAREMA Elisha Nelson Mnyawi amesema kampuni ya God Charity imejitolea kisima kimoja kilichopo kwenye machimbo ya madini ya Tanzanite ili kiwahudumie wachimbaji.
