Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na wananchi wa Mariwanda, akiwa katika ziara ya kikazi Februari 26.2024. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiwa katika picha ya pamoja na wanafunzi wa shule ya msingi Sabasita, iliyopo Bunda Mkoani Mara, wakati alipokua kwenye ziara yake mkoani humo, Februari 26, 2024. Wanafunzi hao wamemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuridhia kutoa fedha za ujenzi wa shule hiyo ambayo imeondoa changamoto ya kusafiri umbali mrefu kufuata huduma ya elimu. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akikagua moja ya darasa la awali katika shule ya msingi Sabasita iliyopo Bunda Mkoani Mara, wakati alipokua kwenye ziara yake mkoani humo, Februari 26, 2024. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiangalia moja ya zana ya kufundishia, wakati alipokagua moja ya darasa la awali katika shule ya msingi Sabasita iliyopo Bunda Mkoani Mara, wakati alipokua kwenye ziara mkoani humo, Februari 26, 2024. Kulia ni Mwalimu Mkuu wa shule hiyo Gatrida Maregesi. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa shule ya msingi Sabasita iliyopo Bunda Mkoani Mara, akiwa kwenye ziara yake mkoani humo, Februari 26, 2024. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiweka jiwe la msingi baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa shule ya sekondari ya wasichana ya Mara Februari 26, 2024. Mheshimiwa Majaliwa amewataka wajenzi wa shule hiyo kufanya kazi usiku na mchana ili iweze kukamilika ifikapo julai 2024 na ianze kupokea wanafunzi. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akikagua maendeleo ya ujenzi wa shule ya sekondari ya wasichana ya Mara Februari 26, 2024. Mheshimiwa Majaliwa amewataka wajenzi wa shule hiyo kufanya kazi usiku na mchana ili iweze kukamilika ifikapo julai 2024 na ianze kupokea wanafunzi. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akikagua maabara katika shule ya sekondari ya wasichana ya Mara, kabla ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa shule hiyo Februari 26, 2024. Mheshimiwa Majaliwa amewataka wajenzi wa shule hiyo kufanya kazi usiku na mchana ili iweze kukamilika ifikapo julai 2024 na ianze kupokea wanafunzi. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiweka jiwe la msingi, wakati alipozindua mradi wa maji Kata ya Sazira Februari 26, 2024. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akifurahia maji, wakati alipozindua mradi wa maji Kata ya Sazira Februari 26, 2024.(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
……….
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza Kamanda wa TAKUKURU Mkoa wa Mara, akamilishe uchunguzi kwenye wizi wa kimtandao unaotumika katika Halmashauri ya Wilaya ya Bunda.
“Kamanda wa TAKUKURU Mkoa fuatilia hili suala kwa haraka, najua mna tabia ya kufanya uchunguzi wenu kwa muda mrefu. Nataka hili likamilike kwa haraka kwa sababu nilishatuma timu yangu na kazi kubwa imeshafanyika.”
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo jioni (Jumatatu, Februari 26, 2024) wakati akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya Mji wa Bunda pamoja na wale wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda uliofanyika kwenye ukumbi wa Herieth, wilayani Bunda mkoani Mara.
Akizungumza na watumishi hao, Waziri Mkuu amesema Serikali ina utaratibu wa kukamilisha matumizi ya fedha zilizopangwa ifikapo Juni 30, kila mwaka. “Ikifika wakati huo, HAZINA wana uwezo wa kuichukua na ikabaki labda iwe imeandikwa barua ya kuombewa kibali maalum cha kuhamisha fedha kwenda mwaka unaofuata.”
“Hapa Bunda mnatumia mwanya huo, kuziombea kibali. Kisha zinahamishiwa kwenye akaunti jumuifu ya amana, halafu zinatolewa na kutumiwa kinyume na utaratibu.”
Amesema mchezo huo unafanywa na watu wachache kwenye Halmashauri ya Wilaya kwa kushirikiana na watumishi wasio waaminifu wa kitengo cha akaunti jumuifu ya amana kilichopo OR-TAMISEMI na hata Katibu Mkuu hawezi kujua mchezo huo wala Madiwani pia hawawezi kujua.
“Mara nyingi wanaocheza mchezo huo hapa Bunda, ni Mkurugenzi wa Halmashauri, Mweka Hazina na Mkurugenzi wa Mipango wa Halmashauri. Kwa mfano, mwaka wa fedha 2021/2022 waliomba kibali cha kuhamisha sh. milioni 871.4 ili ziweze kutumika baada ya muda. Lakini walihamisha sh. milioni 962 na kuzihifadhi huko.”
“Mbali na hizo, kupitia mawasiliano baina ya hawa watatu na wenzao wa TAMISEMI, zikaingizwa tena sh. milioni 215.3. Je ninyi Waheshimiwa Madiwani mliziomba hizo fedha? Je mlijulishwa kwamba kuna fedha za ziada zimeombwa?” alihoji Waziri Mkuu na kujibiwa hapana na madiwani waliokuwepo.
Waziri Mkuu amesema kibaya zaidi, fedha hizo zinapotoka, zinaelekezwa kwenye kazi ambazo tayari zilishatengewa vifungu na ambazo tayari ziliombewa kibali. “Walitoa fedha na kuandika zimetumika kwenye jengo la utawala, kutengeneza fedha za hesabu za mwaka, jengo la wagonjwa wa dharura, posho ya kujikimu ya walimu wapya wa shule za msingi. Hizi zote zilikuwa na fedha zake, je zimeenda wapi?”
“Kamanda wa TAKUKURU, nataka ufuatilie ni nani aliomba hizo sh. milioni 215.3? Ni kwa nini fedha hizi zitumike kwenye kazi ambazo tayari zina mafungu yake? Je ni kweli hawa walimu walilipwa hizo posho? Kwa nini madiwani hawakujulishwa kuhusu mchakato wa fedha hizi?”
Waziri Mkuu anaendelea za ziara yake mkoani Mara kwa kuhutubia wakazi wa Mji wa Bunda.