Na John Bukuku, Dar es Salaam

Ziara ya kitaifa ya Rais wa Singapore, Mheshimiwa Tharman Shanmugaratnam, nchini Tanzania kuanzia tarehe 8 hadi 10 Juni 2026 nalitazama kama tukio la kimkakati lenye uzito mkubwa katika kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na kiuchumi kati ya mataifa haya mawili, ambayo kijiografia yako mbali lakini kimaendeleo na maslahi ya kiuchumi yanaendelea kukaribiana kwa kasi.

Kwa mujibu wa taarifa rasmi iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ziara hiyo inafanyika kwa mwaliko wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha diplomasia ya uchumi inayolenga kuvutia uwekezaji, kuongeza kasi ya biashara na kuimarisha ushirikiano katika teknolojia za ubunifu na maendeleo endelevu.

Umuhimu wa ziara hii unaongezeka zaidi kutokana na ukweli kwamba Mheshimiwa Tharman Shanmugaratnam anakuwa kiongozi wa kwanza wa ngazi ya juu kutoka Singapore kufanya ziara ya kitaifa nchini Tanzania tangu nchi hizi zilipoanzisha uhusiano wa kidiplomasia mwaka 1980. Hii ni hatua inayobeba uzito wa kihistoria na kisiasa katika safari ya miaka 45 ya ushirikiano baina ya pande hizo mbili.

Hali hii inaashiria mabadiliko ya mwelekeo wa uhusiano wa muda mrefu ambao kwa miaka mingi umejikita zaidi katika ushirikiano wa kiufundi, mafunzo na miradi ya kiwango cha wastani cha kiuchumi, lakini sasa ukielekea katika ushirikiano wa kimkakati wenye athari pana zaidi za kiuchumi na kijamii.

Katika muktadha wa sasa wa uchumi wa dunia unaobadilika kwa kasi, Tanzania imeendelea kuweka msisitizo katika kuvutia wawekezaji kutoka Asia, hususan katika sekta za bandari, usafirishaji, nishati, utalii, kilimo na uchumi wa kidijitali, ambapo Singapore imeibuka kuwa mshirika muhimu kutokana na uzoefu wake mkubwa katika usimamizi wa bandari, huduma za kifedha na mifumo ya biashara ya kimataifa.

Taarifa zinaonesha kuwa katika miaka ya hivi karibuni, ushirikiano wa kiuchumi kati ya Tanzania na Singapore umeanza kuonyesha matokeo chanya, ambapo takribani wawekezaji 32 kutoka Singapore wamewekeza nchini Tanzania, wakiwa na thamani ya zaidi ya dola za Marekani milioni 500 na kutoa ajira kwa zaidi ya watu 3000, jambo linalodhihirisha kuimarika kwa imani ya wawekezaji kutoka nchi hiyo.

Hii ni ishara kuwa Singapore inazidi kujijengea nafasi kama mshirika wa kimkakati katika safari ya Tanzania ya kujenga uchumi wa viwanda, kuongeza uzalishaji na kuimarisha sekta za huduma, hususan kupitia teknolojia ya kisasa na ubunifu.

Katika ziara hiyo, ajenda kuu ya mazungumzo kati ya viongozi hao wawili inatarajiwa kujikita katika maeneo ya biashara na uwekezaji, maendeleo ya bandari na usafirishaji, uchumi wa kidijitali, elimu na mafunzo ya ujuzi, nishati, pamoja na miundombinu na teknolojia.

Uwepo wa ujumbe mkubwa kutoka Singapore unaojumuisha mawaziri, maafisa waandamizi wa serikali na wafanyabiashara unaonesha wazi kuwa ziara hii haibebi tu uzito wa kidiplomasia, bali pia ni jukwaa muhimu la diplomasia ya uchumi na uhamasishaji wa uwekezaji wa moja kwa moja.

Kwa upande wa Tanzania, maandalizi ya ziara na mazungumzo haya yanaongozwa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kupitia Waziri Mahmoud Thabit Kombo, jambo linalodhihirisha dhamira ya serikali kuipa kipaumbele sekta ya diplomasia ya uchumi katika sera zake za maendeleo.

Aidha, ziara hiyo inatarajiwa kufungua milango ya mikataba mipya ya uwekezaji na kuharakisha makubaliano muhimu, yakiwemo yale ya ushirikiano wa kodi na ulinzi wa uwekezaji, hatua ambazo zinaweza kuongeza uaminifu na ushirikiano wa muda mrefu kati ya nchi hizo mbili.

Katika upande wa Zanzibar, sehemu ya ziara hiyo itahusisha mazungumzo kati ya Rais wa Singapore na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, jambo linaloonesha kuwa ushirikiano huu unagusa pia mwelekeo mpana wa Muungano na maendeleo ya visiwani.

Ziara hii inatarajiwa kufungua ukurasa mpya katika historia ya mahusiano ya Tanzania na Singapore, kwa kujenga msingi imara wa ushirikiano wa kimkakati unaolenga si tu biashara na uwekezaji, bali pia uhamishaji wa teknolojia za ujuzi na maendeleo endelevu yenye manufaa kwa wananchi wa pande zote mbili.