Na Mwandishi wetu, Simanjiro
MKUU wa Mkoa wa Manyara, Queen Cuthbert Sendiga, amesema Mkoa huo umenufaika kwa miradi mbalimbali ya maendeleo ya kiasi cha shilingi bilioni 790 tangu Rais Dkt Samia Suluhu Hassan aingie madarakani.
RC Sendiga ameeleza hayo kwenye ziara ya Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kenan Laban Kihongosi katika Wilaya ya Simanjiro wakati akihitimisha ziara yake ya siku tatu Mkoani Manyara.
Ameeleza kwamba tangu Rais Dkt Samia aingie madarakani Mkoa wa Manyara umenufaika na miradi mbalimbali ya maendeleo ya kiasi hicho cha shilingi bilioni 790.
Ametaja baadhi ya miradi mbalimbali ya maendeleo iliyofanikiwa kwa fedha hizo katika Mkoa wa Manyara ni kwenye sekta ya afya, elimu, maji, miundombinu na mingineyo.
“Tunamshukuru mno Mheshimiwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan, kwa kusababisha sisi wana Manyara tutembee kifua mbele kwa miradi mbalimbali baada ya kutupatia fedha za maendeleo,” amesema RC Sendiga.
Hata hivyo, RC Sendiga ameeleza kuwa katika mwaka huu wa fedha wa 2026/2027 Mkoa wa Manyara, unatarajiwa kunufaika na miradi ya maendeleo ya shilingi bilioni 300.6.
Kwa upande wake, Katibu wa NEC, Itikadi Uenezi na Mafunzo Kenani Laban Kihongosi amempongeza RC Sendiga kwa namna anavyoongoza Mkoa huo wa Manyara.
“Wana Manyara endeleeni kumpa ushirikiano wa kutosha RC wenu Mhe. Sendiga nafahamu utendaji wake kwani kabla ya kushika nafasi hii nami nilikuwa RC tulikuwa wote,” amesema Kenani.
