Afisa tarafa wa wilaya ya Ilemela Godfrey Mzava akifungua jengo la maliwato lililojengwa Kwa ufadhili wa kanisa la TAG Ilemela kupitia Shirika la Kimisheni la Emmanuel International
……………………
Serikali imelipongeza na kushukuru kanisa la Tanzania Assemblies of God TAG kwa kushirikiana na Shirika la Kimisheni la Emmanuel International kwa kuchangia ukarabati wa vyoo vya zamani vya shule ya sekondari Bugogwa na kujenga vyoo vipya pamoja na ununuzi wa Tanki la Maji vitakavyotumiwa na wanafunzi wa shule hiyo kama sehemu ya mchango wao katika kuchochea maendeleo
Akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa mradi huo mwakilishi wa Mkuu wa wilaya ya Ilemela Mhe Hasan Elias Masala ambae ni Afisa tarafa wa wilaya hiyo Ndugu Godfrey Mzava amelipongeza kanisa kwa kazi nzuri inazozifanya ikiwemo ujenzi wa maadili, usalama na ulinzi pamoja na kuchangia maendeleo
“Zamani kanisa lilijikita kwenye ujenzi wa maadili na kiroho lakini sasa linachangia maendeleo kama hapa Bugogwa wametujengea vyoo , “Alisema
Aidha Gavana Mzava amewataka walimu na wanafunzi wa shule ya sekondari Bugogwa kuhakikisha wanatunza na kuilinda miundombinu hiyo Ili iweze kuleta tija iliyokusudiwa
Kwa upande wake Mwenyekiti wa makanisa ya kipentekoste CPCT Ilemela Mchungaji Ezekiel Motto amefafanua kuwa kanisa la Igombe Christian Center TAG linaunga mkono juhudi zinazofanywa na Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt Samia Suluhu Hasan na kwamba wamefanya ukarabati wa maliwato zenye jumla ya matundu 34 katika shule za msingi Bugogwa, Igombena Kisundi, ukarabati wa Tanki la Maji lenye ujazo wa zaidi ya Lita 10,000 katika shule ya msingi Bugogwa, sambamba na maliwato ya shule ya sekondari Bugogwa yenye matundu 13 pamoja na ujenzi wa maliwato mpya yenye matundu 10 huku jumla ya shilingi milioni 70 ikitumika kugharamia miradi yote iliyotelelezwa
Askofu Rodrick Shoo wa kanisa la TAG Mwanza Kaskazini ametoa wito kwa taasisi na wadau mbalimbali wa maendeleo kuendelea kujitokeza kuunga mkono juhudi za Serikali na kwamba Serikali peke yake haitaweza kutatua kero na changamoto zote zinazokabili wananchi
Nae kiongozi wa wanafunzi wa shule ya sekondari Bugogwa dada mkuu Monica Lucas Chacha amelishukuru kanisa kwa kufanya ukarabati na ujenzi wa matundu ya vyoo katika shule yao na kwamba kabla ya kukamilika kwa maliwato hiyo walikuwa wakikabiliwa na changamoto kubwa ikiwemo kuchelewa vipindi darasani sababu ya kusubiriana kuingia maliwatoni, kuambukizana magonjwa pamoja na kushindwa kuendelea na masomo Kwa wakati sababu ya kuchafuka
Akihitimisha Makamu Mkuu wa shule ya sekondari Bugogwa Mwl Wilson Lusungu Mbunde ameahidi kuvitunza na kuvilinda vyoo hivyo na kuwashukuru Shirika la Kimisheni la Emmanuel International kwa misaada mbalimbali wanayoitoa katika shule yake