Na Sophia Kingimali.
KATIBU Mkuu wa Wizara ya Fedha Dk.Natu Mwamba amesema nchi imejipanga kukuza na kuendeleza kilimo kwa asilimia 10 ifikapo mwaka 2030 na kuajiri vijana milioni 1.5 katika sekta hiyo.
Hayo ameyasema leo februari 9,2024 jijini Dar es salaam wakati akifungua mkutano wa majadiliano ya kimkakati ngazi ya wataalamu mwaka 2024 na kuelekea dira ya Taifa ya Maendeleo mwaka 2050.
Amesema kuwa kutokana na jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk.Samia Suluhu Hassan ambayo imewekeza katika kilimo imepelekea bajeti ya kilimo imeongezeka maradufu.
“Tumeona serikali ilivyowekeza kwa kiasi kikubwa kwenye kilimo lengo kuwaingiza vijana wengi kwenye sekta hiyo ili waweze kujiajiri lakini pia kufikia lengo la nchi la kujitisheleza kwa chakula na kulisha Dunia ndio maana Rais wetu ameweka pesa nyingi kwenye kilimo ikiwemo mradi BBT”amesema
Amesema Tanzania ina uwezo mkubwa wa kutoa nafaka nyingi na kuweza kulisha ndani na nje ya nchi za jirani ,hivyo kwa upande wa kilimo litajadiliwa kwa kina ili kuweza kufikia malengo endelevu.
Amesema kuwa matokeo ya mkutano huo yataweza kujenga vizuri mambo ya kimaendeleo yanayokusudiwa kufanya katika maeneo matano ikiwemo rasilimali watu,miundombinu,kilimo na mifumo ya fedha .
“Mjadala huu wa kimkakati wa ngazi ya kiufundi wa mwaka 2024 ni muhimu sana kwani mijadala itahusu maeneo mbalimbali ya mada ambayo tunatarajia yatakuwa na mapendekezo yatakayochochea utekelezaji wa vipaumbele”amesema.
Ameongeza kuwa,kwa kuzingatia hilo mijadala yao itazingatia uwekezaji wa kimkakati mifumo ya sera na uthibiti na mipango shirikishi iliyoundwa ili kuboresha muunganisho na kuboresha ufikiaji wa huduma muhimu na kuunda mazingira wezeshi kwa maendeleo endelevu.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Mashirika yasiyo ya kiserikali AZAKI NaCoNGO Dk.Lilian Badi amesema wao kama baraza wameanza kutoa mchango katika kuhakikisha dira hiyo inazingatia suala zima la maendeleo jumuishi hususani ushiriki wa makundi maalum katika shughuli za kiuchumi na huduma za jamii zinazopewa kipaumbele katika utekelezaji wa hatua mbalimbali za Serikali na wadau wake.