Na: Dk. Reubeni Michael Lumbagala, Kongwa.
NIANZE kwa kuuliza swali; Tunataka ushahidi gani juu ya uwezo wa wanawake katika uongozi?
Nimeamua kuanza na swali hili kutokana na dhana potofu ambayo ninaamini bado imo kwa baadhi ya watu kwamba wanawake hawana uwezo wa kumudu majukumu ya uongozi.
Dhana hii imepata nafasi na kuishi nayo kwenye baadhi ya myoyo ya watu wetu kutokana na historia ya jamii zilivyokuwa zikimchukulia mwanamke kwa muda mrefu.
Jamii nyingi duniani, si Tanzania pekee, kwa muda mrefu zimemchukulia mwanamke kama kiumbe dhaifu, asiyekuwa na uwezo wa kufanya yale ambayo wengi wamezoea kuona yakifanywa na wanaume na kwamba mahala pake ni jikoni au chumbani ‘akimpumbaza’ mumewe baada ya kazi na kulea watoto.
Lakini wataalamu wa mambo ya jinsi na jinsia wanatufundisha kwamba kunachomtofautisha mwanaume na mwanamke ni vitu takribani vitatu tu, basi.
Kwa upande wa mwanamke wataalamu wanasema asichoweza kufanya ni kitu kimoja tu, kwamba hawezi kutia mimba, basi, lakini taja vingine vyote utakavyotaja anaweza. Utake huo ndio ukweli na usitake ndio hivyohivyo!
Kwa upande wa mwanaume kuna vitu viwili tu ambavyo mwanamke anaweza lakini yeye mwanaume hawezi; kubeba mimba na kunyonyesha.
Ukija kwenye majukumu mengine ya kijinsia wote, mwanamke na mwanaume sawa kama nilivyokwisha dokeza. Kwa mfano, nani alikwambia mwanaume hawezi kupika wakati mkewe akitazama TV, kwamba mwanaume hawezi kufua nguo, kutandika kitanda na shughuli nyingine ambazo jamii yetu imejengwa kuamini kwamba ni kazi za kike?
Toka umezaliwa, ni mwanaume gani uliwahi kusikia kwa sababu ya kupika, kufua, kubeba mtoto au kudeki nyumba maumbile yake ya kiume, labda tuseme, ashakum si matusi, korodani zilitoweka? Hakuna.
Kwa hiyo kama ilivyo ukweli kwamba mwanamke anaweza kuchimba dhahabu, kubeba zege, kuendesha ndege, kuwa daktari wa meno au kazi yoyote utakayotaja ndivyo pia anavyoweza uongozi.
Kwa miongo mingi, dhana hii ya kumwona mtoto wa kike ni mtu wa kuolewa na shughuli zake ni jikoni imetuchelewesha sana kimaendeleo.
Kwa muda mrefu, hata haki ya kupata elimu, wasichana walinyimwa. Ungesikia mzazi akisema, “Mimi nisomeshe mtoto wa kike wa kazi gani?”
Kwa hiyo, kunyimwa haki ya kupata elimu kumeendelea kwa muda mrefu kuwarudisha nyuma kimaendeleo wasichana na wanawake.
Hata baadhi ya wanawake waliobahatika kusoma, kujiajiri au kuajiriwa, waume zao waliwakataza kufanya kazi ambayo ingemsaidia kuongeza kipato cha familia. Ujinga kweli kweli.
Kadri miaka ilivyokwenda, jamii zilianza kubadilika hata kama si kwa kasi sana. Taratibu wanawake ambao ndio wengi kwa idadi kuliko wanaume wakaanza kuaminika, wakapewa fursa ya kupata elimu na kufanya kazi ambazo awali iliaminika hawawezi kuzifanya.
Kwenye uongozi, wanawake pia walianza kuaminika kwa kuteuliwa na kuchaguliwa katika nafasi mbalimbali japo huku kwenye kuchaguliwa bado kuna kazi ya kufanya.
Kazi haijafanyika vya kutosha ili jamii kujitenga na ‘mtazamo-dume” ndio maana bado bungeni tuna wabunge wengi wanaume wa kuchaguliwa kulinganisha na wanawake. Inatakiwa tufikie mahala tuachane na viti maalumu.
Pamoja na kwamba tupo kwenye karne ya ishirini na moja, yenye mabadiliko makubwa kuhusiana na uwezo wa wanawake, wapo baadhi wa watu wanaishi kwenye karne ya ishirini na moja lakini wakiwa na mawazo ya karne ya kumi. Hili nalo ni tatizo kubwa ambalo hata makala yanalenga kulimaliza.
Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson ni miongoni mwa wanawake ambao ni chachu na darasa tosha la kubadili dhana dhana potofu kwa baadhi ya watu ndani na nje ya nchi yetu kuhusu uwezo wa wanawake katika uongozi.
Yeye alifanikiwa kuwa spika mwanamke wa pili katika Bunge letu la Tanzania, si kwa upendeleo wowote bali uwezo.
Hii imethibitisha uwezo mkubwa walionao wanawake kushika nafasi nyeti kama hiyo ya mhimili wa Bunge ambao una dhima ya kutunga sheria, kupitisha bajeti za serikali, kuihoji serikali na kuielekeza la kufanya kwa niaba yetu sisi wananchi.
Oktoba 27, 2023, Spika Dk. Tulia aliendelea kuwa darasa zuri la kuuthibitishia ulimwenguni juu ya uwezo wa wanawake katika uongozi kwa kushika nafasi nyeti duniani baada ya kuchaguliwa kuwa Rais wa 31 wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU).
Uchaguzi huo ulifanyika Luanda, nchini Angola ambapo Dk. Tulia alitangazwa mshindi kwa kupata kura 172 kati ya kura 303 zilizopigwa.
Wengine waliochuana na Dk Tulia ni pamoja na Adjidiarra Kanoute wa Senegeal aliyepata kura 59, Catherine Hara wa Malawi aliyepata kura 61 na Marwa Hagi wa Somalia aliyepata kura 11.
Kabla ya uchaguzi huo, Dk. Tulia alitaja vipaumbele vyake ikiwemo kuimarisha uwazi na uwajibikaji katika bunge hilo na kuimarisha amani na ustawi wa IPU kimataifa.
Vilevile alisema atastawisha ushiriki wa makundi mbalimbali katika siasa kwenye Bunge la IPU, mathalani makundi ya wanawake, vijana na makundi mengine yasiyo na uwakilishi.
Katika kukazia sera zake, Dk. Tulia alisema “Mbali na vipaumbele nilivyovitaja, uongozi wangu utakwenda kutekeleza mikakati ya IPU ya 2022-2026 ya kujenga bunge imara na lenye nguvu, kukuza ushirikishwaji na uwakilishi ndani ya bunge.”
Ushindi wa Dk. Tulia ni kielelezo muhimu kuwa wanawake wanaweza kumudu majukumu makubwa pengine kuzidi hata wanaume.
Kuaminiwa kwa daktari huyu wa falsafa za sheria kuongoza taasisi hii muhimu yenye maspika wa bunge 120 kutoka nchi mbalimbali duniani, kunazidi kuitangaza Tanzania kimataifa.
Pamoja na hilo, kunazidisha ujenzi wa mahusiano mazuri ya Tanzania na mataifa mengine ulimwengu na hivyo kuchagiza mafanikio ya mipango na mikakati ya kimaendeleo tuliyonayo inayohitaji ushirikiano na mataifa mengine ulimwenguni.
Rais Samia Suluhu Hassan ambaye pia ni mwanamke anayezidi kudhihirisha uwezo mkubwa wa uongozi walio nao wanawake aliompongeza Spika Tulia kwa kuchaguliwa kuwa Rais IPU.
“Kuchaguliwa kwako pia ni matokeo ya miaka mingi ya kazi, weledi na kujituma katika utumishi wa umma, mfano bora kwa watoto wa kike katika nchi yetu, Afrika na hata nje ya mipaka ya bara letu,” amesema Rais Samia.
Watanzania tubadilike sasa. Tuamini wanawake wanaweza kumudu majukumu ya uongozi.
Lakini ni muhimu kuweka angalizo kwa wasichana na wanawake kufahamu kuwa hawatakubalika na kuaminika kwenye nafasi za uongozi kwa kwa sababu ya jinsi zao pekee, bali kwa uwezo, maarifa, uzoefu, uadilifu na uzalendo walionao katika nchi na kazi.
Dk. Tulia anaingia kwenye historia kubwa ulimwenguni ambapo anakuwa mwanamke wa kwanza kuongoza bunge hilo lenye nchi wanachama 179 na wabunge 705 wanaoziwakilisha nchi zao.
Ni kwa mantiki niungane na wengine kukupongeza kwa dhati kabisa Dk. Tulia kwa kuaminiwa katika nafasi hiyo. Mungu akutangulie, akusaidie na kukuwezesha kwenye majukumu mapya.
Shime wazazi na taifa kwa ujumla tuendelee kuwajenga na kuwaibua akina Dk. Tulia wengi zaidi.
Dk. Reubeni Michael Lumbagala ni Mwalimu wa Shule ya Sekondari Mlali iliyoko wilaya ya Kongwa-Dodoma. Maoni: 0620 800 462.