Na Albano Midelo,Songea 

MKATABA wa ujenzi wa kiwanda kikubwa cha sukari  chenye thamani ya shilingi bilioni 500  ambacho kinajengwa katika Kijiji cha Magwamila Kata ya Lilai Muhukuru wilayani Songea mkoani Ruvuma umesainiwa kwenye ukumbi wa Mkuu wa Wilaya Songea Januari 23,2024.

Mkuu wa Wilaya ya Songea Mheshimiwa Kapenjama Ndile amesema mkataba huo ni makubaliano ya awali baina ya viongozi wa Kijiji cha Magwamila na wawakilishi wa Songea Sugar Limited  ambayo ni tawi la kiwanda cha Kagera Sugar ambao hivi sasa wamewekeza nchini Uganda  na  wameamua kuanzisha tawi la kiwanda hicho mkoani Ruvuma .

“Mkataba umeshuhudiwa na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Songea,Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma na wawakilishi kutoka Kituo cha Uwekezaji Tanzania Kanda ya Nyanda za Juu Kusini  chenye makao makuu yake jijini Mbeya’’.alisisitiza DC Ndile.

Ndile amewataka wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea na Mkoa wa Ruvuma kwa ujumla kujiandaa kuupokea uwekezaji wa kiwanda kikubwa cha sukari katika Katika Kijiji cha Magwamila.

Amesisitiza kuwa  wawekezaji  hao wanatarajia kuweka zaidi ya bilioni 500 katika kiwanda hicho, ambapo kiwanda kitazalisha tani zaidi ya laki moja kwa mwaka.

 Ameongeza kuwa kiwanda hicho kitaweza kuzalisha umeme ambao utaweza kuuzwa kwenye grid ya Taifa, pia kitazalisha mafuta aina ya ethane ambapo amesema kuwepo kwa kiwanda hicho kitaleta manufaa makubwa katika  wilaya ya Songe ana Mkoa wa Ruvuma kwa ujumla.

Kwa upande wake  Mchumi Mwandamizi wa Bodi ya Sukari Tanzania Joshua Mhando ameishukuru Serikali inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuweka mazingira wezeshi kwa wawekezaji.

Naye Mwakilishi wa Mwekezaji wa kiwanda hicho, Kapil Dave ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania kwa kuweka utaratibu mzuri wa uwekezaji ambapo ameahidi kufanya uzalishaji wenye tija na wenye kuleta maendeleo chanya.

Eneo la uwekezaji wa kiwanda cha sukari linatarajiwa kuwa na ukubwa wa hekta 30,000 kati ya hizo hekta 22,000 zitakuwa kwa ajili ya kilimo cha miwa na hekta 8,000  kwa ajili ya ufungaji wa mitambo ya kiwanda, barabara za ndani, maghala, makazi ya watumishi, ujenzi wa huduma za kijamİi.

Picha ya kwanza na ya pili ni matukio ya kusaini mkataba wa makubaliano ya ujenzi wa kiwanda kikubwa cha sukari chenye thamani ya shilingi bilioni 500 katika kijiji cha Magwamila wilayani Songea mkoani Ruvuma.Mkataba huo umesainiwa baina ya viongozi wa kijiji cha Magwamila na wawakilishi wa wa wawekezaji kutoka nchini Uganda 

Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas ambaye amekuwa mstari wa mbele kuhamasisha wawekezaji kufika kuwekeza mkoani Ruvuma ambako kuna fursa nyingi za uwekezaji