NA DENIS MLOWE, IRINGA
Kampunk ya Qwihaya General Enterprises Co. Ltd imeng’aa baada ya kunyakua Tuzo la kuwa mlipa kodi Bora kwa mwaka 2023.
Qwihaya imepatiwa tuzo hizo na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) katika hafla iliyofanyika Disemba 7, 2023 Mkoani Iringa.
Mwenyekiti wa Qwihaya Group, Leonard Mahenda Qwihaya (MNEC) amesema ulipaji wa kodi ni muhimu kwa sababu hakuna Maendeleo kwenye Taifa kama kodi hailipwi.
“Tutaendelea kulipa kodi bila kusukumwa kwa sababu kodi ndio uchumi wa Taifa letu,” amesema Qwihaya.
Awali Mkuu wa Mkoa wa Iringa Halima Dendego aliwapongeza walipa kodi waliopata tuzo kwa mwaka 2023.
“Serikali itaendelea kuweka mazingira mazuri kwa wafanyabiashara wote kwa sababu lengo letu ni kuona wanafanikiwa lakini pia na serikali yetu ifanikiwe,” amesema Dendego.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Peris Mugiri aliwahimiza wafanyabiashara kuendelea kulipa kodi.
“Niwahimize endeleeni kuunga mkono TRA na Serikali yetu kwa sababu kodi ndio mambo yote, ukiona tunapata huduma za kijamii na miradi inatekelezwa ni kwa sababu ya kodi,” amesema Magiri