Baadhi ya wakazi wa mtaa wa Yespa Manispaa ya Morogoro wakiwa njee wa nyumba zilizozingirwa na maji.
……………………………………..
NA FARIDA SAIDY, MOROGORO
Baadhi ya kaya zilizo kandokando ya Mto Ngerengere Mtaa wa Yespa Manispaa ya Morogoro zimezingirwa na maji na kusababisha wakazi wa mtaa huu kuhama kwa muda, ambapo imeelezwa hali hiyo imesababishwa na Maji kupoteza mwelekeo baada ya sehemu ya mto kuzibwa katika ujenzi wa Reli ya kisasa.
Wakiongea kwa nyakati tofauti wakazi hao wamesema kuwa hali hiyo imesababishwa na maji kupoteza mwelekeo kufuatia ujenzi wa miundombinu ya reli ya kisasa ambao imesababisha maji kujaa katika makazi ya watu.
Aidha wakazi hao wamesema kuwa hali hiyo ya maji kuingia kwenye maeneo ya makazi imetajwa kusababisha hasara, ambapo licha ya baadhi ya watu kulazimika kuyahama makazi yao kwa muda, pia baadhi ya huduma zimesimama ikiwemo ibada.
Wakazi hawa walio pembezoni mwa mto Ngerengere wamesema kuwa wengi wao wameishi kwa muda mrefu katika maeneo hayo lakini wajawahi kukutana na changamoto ya kuzingirwa na maji hivyo swala hilo kwao wanaliona ni tatizo hivyo wanaiomba mamlaka husika kulichulia hatua.
Pamoja na kaya zilizo zingirwa na maji kuwa pembezoni mwa mto Ngerengere, Malalamiko ya wakazi hao ni ujenzi wa Reli ya kisasa, wakidai sehemu kubwa ya mto imezibwa ambapo kufuatia mvua zinazo endelea kunyesha mto huo umefurika na maji kusambaa baada ya kukosa mwelekeo.