Na. Asila Twaha, OR -TAMISEMI
Katibu Tawala wa Mkoa wa Tabora Dkt. John Mboya amewataka Maafisa Tarafa na Watendaji wa Kata kuijua na kuisimamia miradi ya maendeleo ambayo ipo katika maeneo yao sababu fedha nyingi za miradi zinapelekwa kwenye ngazi ya msingi ya maeneo yao.
Dkt. Mboya amesisitiza hayo Novemba 26, 2023 wakati akifungua Mafunzo ya Kuwajengea uwezo Maafisa Tarafa na Watendaji wa Kata wa Mkoa wa Tabora yenye lengo la kuwakumbusha utekelezaji wa majukumu yao kwa kuzingatia misingi ya Sheria,Taratibu, Kanuni na Miongozo ya kazi zao.
Amesema fedha nyingi za miradi zinapelekwa na Serikali katika kata ambako ndiko kwenye ngazi za msingi ya utekelezaji wa miradi hiyo kama maji, afya na elimu kwa ajili ya wananchi lakini utakuta mradi haujakamiliki na Afisa huyo hafuatilii na hajui kitu chochote sababu ya mradi kutokamilika.
“ Afisa Tarafa au Kata hivi upo kwenye Kata kwa kazi zipi kama sio kazi ya kuisaidia Serikali” Dkt. alisema Mboya
Dkt. Mboya amewataka Maafisa hao kutambua nafasi walizokuwanazo katika maeneo yao kwa kufanya kazi kwa kujituma, kufuatilia maendeleo ya miradi na pia katika utatuzi wa kero za wananchi ili kumsaidia Mkurugenzi kwa kutatua kero zinazowakabili wananchi wa maeneo yao husika.
“msisubiri mpaka viongozi wa ngazi za juu waje katika maeneo yenu ndio wananchi waeleze kero zao na wewe upo pale unaweza kusikiliza na kutatua na tunaamini kama huwezi unajua wapi upeleke ili zishughulikiwe” amesisitiza Dkt. Mboya.
Aidha, amewataka Maafisa hao kutokukaa ofisini na kutakiwa kuenda kuwafuata wananchi kwa kuwasikiliza kero zao na kushaurina nao ili kuleta maendeleo katika maeneo yao.
Naye Mkufunzi na Mkuu wa Idara ya Mafunzo ya Muda Mfupi,Tafiti na Shauri za Kitaalamu Chuo cha Utumishi wa Umma Hosea George ametoa wito kwa maafisa hao kuwa waadilifu na kuwa watumishi waaminifu kwa kufanya kazi kwa misingi ya utumishi bora sababu amesema, utumishi wa umma ni pamoja na matendo na tabia iliyonjema.
Aidha, amesema haipendezi kwa mtumishi na wala haitakiwi kuwa na vitendo visivyofaa vya kutaka au kuchukua rushwa, ulevi, mavazi yasiyoridhisha na kauli sisizofaa kwa jamii inayo kuzunguka kwani tabia hiyo inapelekea watu unaowahudumia kukosa imani kwao na Serikali yao.