Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt Mwigulu Lameck Nchemba(Mb) akieleza dhamira ya Serikali ya kuwalipa wakandarasi wakati wa Mkutano wa Mashauriano kati ya Serikali na Makandarasi wazawa, Washauri elekezi pamoja na wadau mbalimbali wa Sekta ya Ujenzi ulioangazia kujadili nafasi yao katika Utekelezaji wa Miradi ya Sekta ya Ujenzi, uliofanyika katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete Convention Center jijini Dodoma.
…………………………
Serikali imeweka kwenye Sheria kiwango cha thamani ya miradi iliyokuwa ikitekelezwa na wazawa kutoka shilingi bilioni 10 hadi shilingi bilioni 50 ili kuwawezesha wazawa kunufaika na kuwafanya wawe walipakodi wakubwa kwa maendeleo ya nchi.
Hayo yameelezwa jijini Dodoma na Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) wakati wa Mkutano wa Mashauriano kati ya Serikali, Makandarasi na Washauri Elekezi wa Ndani ulioangazia nafasi yao katika utekelezaji wa miradi.
“Sheria ilikuwa inawapa local content Wakandarasi bora ambao ni wazawa lakini kwa sasa wazawa wanaruhusiwa kupata mradi wenye ukubwa wowote na kuruhusiwa kuajiri wakandarasi wengine kutoka nje kwa miradi wanayotekeleza.
Kuhusu malipo ya Wakandarasi, Dkt. Nchemba alisema kuwa kila mwaka Serikali inatenga fedha za kulipa madeni na miradi inayoendelea ambapo inatenga zaidi ya shilingi bilioni 600 kwa ajili ya kuwalipa Wakandarasi, watoa huduma na wazabuni na hivyo kuwataka wanaoidai Serikali kuwa wavumilivu wakati jitihada za kuwalipa zikiendelea.
Kwa upande wake Waziri wa Ujenzi, Mhe. Innocent Bashungwa, amesema kuwa katika mwaka wa Fedha 2023/2024 kazi zote za matengenezo ya Barabara zinazosimamiwa na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROAD) kupitia Mfuko wa Barabara kwa mikoa 26 nchini zitatekelezwa na Wakandarasi wa ndani na hilo ni agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Ametoa rai kwa wananchi kuwa wakiona kwenye mikoa kuna wakandarasi wa nje wanafanya kazi hizo kwa fedha za mfuko wa barabara watoe taarifa kwa kuwa watakuwa wamekwenda kinyume na maelekezo ya Serikali.
Naye Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi Bw. Daniel Chongolo, alisema kuwa ni lazima kuaminiana na kuwawezesha wakandarasi wazawa kufanya mambo makubwa kwa kuweka mazingira ambayo yatawafanya makandarasi wazawa kuongeza viwango na kuweza kufanya kazi nje ya nchi kama wakandarasi wa nje wanavyokuja kufanya kazi nchini.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi Bi. Aisha Amour, alisema kuwa Tanzania inajumla ya Wakandarasi 15,665 ambapo wakandarasi wa ndani ni 15,091 ilihali wakandarasi wa nje ni 574 ambapo Kampuni za wakandarasi wanawake ni 1,215.
Aidha wadau wa mkutano huo wameeleza kuwa miradi iliyotekelezwa kuanzia mwaka 2013 hadi 2023 ni miradi 36,839 na kati ya miradi hiyo thamani yake ilikuwa shilingi trilioni 61 ikiwa ni miradi iliyosajiriwa na CRB, kati ya miradi hiyo, miradi 35,351 yenye jumla ya shilingi trilioni 23.75 ndiyo ilitekelezwa na makandarasi wa ndani, hatua iliyosababisha kuwa na mkutano huo ili kujadili namna wakandarasi wazawa wanavyoweza kutumia fursa zilizopo kuongeza kiwango cha ushiriki katika utekelezaji wa miradi mikubwa inayotekelezwa nchini.
Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Bw. Daniel Chongolo, akieleza kuhusu kuwawezesha wazawa katika kutekeleza miradi mikubwa katika Mkutano wa Mashauriano kati ya Serikali na Makandarasi wazawa, Washauri elekezi pamoja na wadau mbalimbali wa Sekta ya Ujenzi uliojadili nafasi yao katika Utekelezaji wa Miradi ya Sekta ya Ujenzi, uliofanyika katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete Convention center jijini Dodoma.
Waziri wa Ujenzi, Mhe. Innocent Bashungwa (Mb) akizungumza kuhusu utekelezaji wa miradi kupitia Mfuko wa barabara, wakati wa Mkutano wa Mashauriano kati ya Serikali na Makandarasi wazawa, Washauri elekezi pamoja na wadau mbalimbali wa Sekta ya Ujenzi ulioangazia nafasi yao katika Utekelezaji wa Miradi ya Sekta ya Ujenzi, uliofanyika katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete Convention Center, jijini Dodoma.
Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt Mwigulu Lameck Nchemba(Mb) na Waziri wa Ujenzi, Mhe. Innocent Bashungwa (Mb), wakizungumza jambo, wakati wa Mkutano wa Mashauriano kati ya Serikali na Makandarasi wazawa, Washauri elekezi pamoja na wadau mbalimbali wa Sekta ya Ujenzi ulioangazia nafasi yao katika Utekelezaji wa Miradi ya Sekta ya Ujenzi, uliofanyika katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete Convention Center, jijini Dodoma.
Wakandarasi kutoka maeneo mbalimbali ya nchi na wadau wengine wakiwa katika Mkutano wa Mashauriano kati ya Serikali na Makandarasi wazawa, Washauri elekezi pamoja na wadau mbalimbali wa Sekta ya Ujenzi ulioangazia kujadili nafasi yao katika Utekelezaji wa Miradi ya Sekta ya Ujenzi, uliofanyika katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete Convention center jijini Dodoma.