Na John Walter-Babati
Wananchi wa kata ya Nkaiti wilaya ya Babati mkoani Manyara wameiomba serikali kuharakisha ujenzi wa mradi wa maji Darakura Minjingu ili waondokane na adha ya ukosefu wa maji.
Mwakilishi wa wananchi katika kata hiyo Mheshimiwa Diwani Steven Mollel amesema Maji wanayotumia kwa sasa yanatokea mto Dagaa ambayo hata hivyo hayana nguvu na kwamba jitihada zilizopo ni kuunganisha na chanzo cha Mayoka ili wananchi waendelee kupata huduma ya maji wakati wakisubiri mradi mkubwa wa Darakuta.
Kwa kuwa jamii ya wanaoishi Nkaiti wengi wao ni wafugaji, Mollel amesema wananchi hulazimika kuchimba visima vifupi ili mifugo ipate maji.
Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira mjini Babati (BAWASA) ambao ndio wasimamizi wa mradi huo Mhandisi Iddy Msuya, amesema mradi ulishaanza ila ulisimama baada ya mkandarasi aliyekuwepo awali kuondolewa kwa kukiuka utaratibu.
Amesema kwa sasa wapo katika hatua ya Ununuzi wa Mabomba na muda wowote Mradi utaendelea ili ifikapo Juni 6,2023 wananchi waanze kufurahia huduma ya maji safi na Salama kupitia mradi huo wa shilingi Bilioni 8