Adeladius Makwega-MWANZA
Wanachuo na Wakufunzi wa Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya wamepata nafasi ya kuuliza maswali juu ya Ukatili wa Kinjinsia hapo chuoni Novemba 16, 2023 baada ya Afisa Ustawi wa Jamii Wilaya ya Kwimba kutembelea Chuo hiki na kutoa mada kadhaa juu ya dhana nzima ya ukatili huo kwa jamii ya Kitanzania .“Je ni kweli mke kumnyima unyumba mumewe ni ukatili wa kijinsia ?”.
Swali hili lilijibiwa kuwa mke anaweza kumfanyia mumewe ukatili wa kijinsia lakini hilo linaweza lisiwe hivyo kutokana na mazingira na hali ya afya ya mke wakati anafanya hivyo.
Akijibu swali hilo ndugu Kayanda Kipole ambaye ni Afisa Utawi wa Jamii Wilaya ya Kwimba alisema,
“Swali hilo linapendwa kuulizwa sana na jamii, dhana ikiwa, bingwa wa ukatili wa kijinsia mara zote huwa ni mwanaume, lakini ukatili unaweza kufanywa na mtu yoyote yule na hata takwimu za wilaya ya Kwimba zinathibitisha hilo. Kama mwanamke hayupo katika dharura hiyo ya mzunguko wa mwezi akawa anatoa visingizio vya kukataa tendo la ndoa mara nyingi na miezi kupita, hapo atakuwa anafanya ukatili wa kijinsia kwa mumewe pasi na shaka yoyote ile.”
Huku wanachuo hao wakisikiliza kwa umakini maelezo ya Afisa Ustawi wa Jamii Wilaya ya Kwimba, mtaalamu huyu wa msauala ya kijamii alisema kuwa kwa sasa hali ya ukatili wa kijinsia imefikia kubaya sana.
“Maana watuhumiwa wanaonekana kuhusika sana na matukio haya ni ndugu na watu wa karibu wa wahanga wengi, watu wa karibu walitakiwa kuwa walinzi wa kwanza wa kila mmoja, Je wnajamii wamkimbilie nani? Kama siyo mimi na wewe? Sasa ni wakati sahihi , sasa ni wakati wa kuamua kubadilika kila mmoja wetu na tusiwe chanzo cha ukatili wa kijinsia kwa yoyote yule aliye mbele yetu na kwa hilo ndiyo maana Serikali imeatuagiza kuzunguka kila kona kutoa elimu hii na leo nipo hapa Malya chuoni kwenu.”
Hali hii inaleta uwoga mkubwa kwa jamii, kwa hiyo jitihada za kila mmoja zinahitajika ili kuweza kupambana na ukatili huo pahala popote katika jamii yetu.
Akizungumza mara baada ya mawasilisho haya, Eliasi Mashenzi ambaye ni Katibu wa Serikali ya Wanachuo ambaye pia ni mwanachuo wa Stashahada ya Michezo mwaka wa pili amesema kuwa wanamshukuru ndugu Kayanda kwa mada yake maana sasa kila mmoja amefahamu nini maana ya ukatili wa kinjinsia na jinsi ya kupambana na hali hiyo katika mazingira ya chuo na hata makazini mara baada ya kuhitimu mafunzo yao.