Na Mwandishi Wetu
TAASISI inayojuhusisha na Utoaji Elimu ya Kisukari kwa Jamii (DICOCO) kwa kushirikiana na Hospitali ya SINAI wametoa huduma ya kupima kisukari, shinikizo la damu na uzito kwa waandishi wa habari ambao ni Wanachama wa Klabu ya Waandishi wa Habari Dar es Salaam(DCPC).
Huduma hiyo imetolewa jana na wataalam wa afya wa taasisi hizi wakati wa Mkutano Mkuu wa mwaka wa DCPC, uliofanyika kwenye Ukumbi wa Anatoglou uliopo wilayani, Ilala mkono humo.
Wanachama wa DCPC wamekutana kwa siku mbili ambapo Oktoba 27 walifanya mkutano na wadau mbalimbali ambao wamechangia mkutano huo na Oktoba 28, 2023 wakafanya mkutano mkuu.
Wakizungumza baada ya kupima magonjwa hayo, waandhishi hao wamesema wanaishukuru DICOCO na Hospitali ya SINAI kuona haja ya kutumia mkutano huo kutoa huduma hizo kwani wameonesha namna ambavyo wanajali kundi hilo ambalo limekuwa na jukumu la kuhabarisha umma kuhusu matukio ya habari nayotokea nchini.
Mwandishi Bakari Kimwanga amesema kuna kila sababu ya waandishi wa habari na jamii kwa ujumla kujenga utamaduni wa kupima afya zao hasa katika nyakati hizi ambazo magonjwa yasiyoyakuambukiza yameendelea kushika kasi.
“Tunashukuru ndugu zetu kutupatia huduma hii, wamefanya jambo kubwa na nzuri na tunasema asante, lakini nitoe rai kwa waandishi wa habari wa mikoa kuwa na utamaduni wa kupima afya zetu, itatusaidia sana kujua afya zetu.”
Kimwanga ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Makurumla na Mhariri Mtendaji wa Best Media amesema ni wazi ili kukabiliana na maradhi yasiyoyakuambukiza ni vema jamii iwe na utamaduni wa kupata taarifa sahihi kuhusu afya zao kwani itasaidia kujikinga ama kuchukua hatua ili kutopata maradhi hayo.
Kwa upande wake Mwandishi Selemani Msuya ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Vyombo vya Habari Tanzania(JOWUTA) amepongeza uamuzi wa DCPC kuwapa nafasi watoa huduma hao kupima afya za waandishi kwani moja ya changamoto kubwa ni waandishi kutokuwa na muda wa kupima afya zao.
“Moja ya changamoto tunayopitia waandishi ni muda wa kupima afya zetu, hivyo nitoe ombi kwa DCPC isisubiri mkutano wa kila mwaka bali ishirikiane na wadau hao kila baada ya miezi mitatu, tuweze kupima afya zetu, ” amesema Msuya.
Awali Mwanzilishi wa Taasisi ya DICOCO, Lucy Johnbosco amesema binafsi amekuwa akiishi na kisukari aina ya kwanza kwa zaidi ya miaka 20 lakini kwa kutambua umuhimu wa kupima afya ameona ni vema taasisi yao ikatoa huduma hiyo bure kwa waandishi wa habari Mkoa wa Dar es Salaam.
“Kwa kuwa leo ni siku ya Mkutano Mkuu wa Klabu DCPC na mimi nikiwa Mwandishi wa habari nilipata wazo moja waandishi wa habari wanakuja kwenye matukio mbalimbali kuchukua habari lakini je afya yao zikoje?
” Walishawahi kupata huduma ya kufanyiwa upimaji sasa nilivyokuwa najiuliza hivyo nikaona siku kama ya leo kwa kuwa inanihusu sio tu kwamba nije kuhudhuria mkutano lakini pia nitoe huduma ya kupima sukari, presha, urefu, uzito na kutoa elimu ya lishe kwa watu wote sio tu kwa mtu ambaye anaishi na ugonjwa wa kisukari kwasababu wanasema maradhi yasiyoyakuambukiza ukipata elimu sahihi na ukafanya vipimo ni rahisi kuepuka kama haujakutwa na magonjwa yasiyoambukizwa…
“Lakini kama ukikutwa nayo na ukapata elimu sahihi ni rahisi kujua ni namna gani unaweza ukaishi na haya maradhi.Kwa hiyo ndio sababu kubwa, lakini waandishi wa habari wanajitoa katika matukio ya wengine lakini je hao wanaondaa matamasha mbalimbali ambayo waandishi wanakwenda kuchukua habari kutoka kwao walishawafikiria waandishi wa habari?
” Na kwa uzoefu wangu waandishi wa habari hatujawahi kufikiriwa, hivyo kwa kuwa mimi ni mwaandishi wa habari na nina taasisi ambayo inaweza kufanya jukumu hili nimeona nije nitoe huduma hii bure kwa ndugu zangu.”