Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni, akizungumza na Mkurugenzi wa Shirika la Kimataifa la Wakimbizi (UNHCR), Kanda ya Mashariki, Pembe ya Afrika na Maziwa Makuu, Clementine Nkweta-Salami (kulia). Mazungumzo hayo yalifanyika katika ofisi ya Naibu Waziri, jijini Dodoma, leo. Wapili kulia ni Mwakilishi Mkazi wa Shirika hilo Nchini, Chansa Kapaya.
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni (kulia), akimsikiliza Mkurugenzi wa Shirika la Kimataifa la Wakimbizi (UNHCR), Kanda ya Mashariki, Pembe ya Afrika na Maziwa Makuu, Clementine Nkweta-Salami, alipokuwa anamfafanulia jambo katika mazungumzo yao yaliyofanyika jijini Dodoma, leo. Kushoto ni Mwakilishi Mkazi wa Shirika hilo Nchini, Chansa Kapaya.
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni (kushoto), akiagana na Mkurugenzi wa Shirika la Kimataifa la Wakimbizi (UNHCR), Kanda ya Mashariki, Pembe ya Afrika na Maziwa Makuu, Clementine Nkweta-Salami, baada ya kumaliza mazungumzo yao yaliyofanyika ofisi za Wizara hiyo, jijini Dodoma, leo. Picha zote na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
Na Mwandishi Wetu, MOHA, Dodoma.
NAIBU Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni amefanya mazungumzo na Mkurugenzi wa Shirika la Kimataifa la Wakimbizi (UNHCR), Kanda ya Mashariki, Pembe ya Afrika na Maziwa Makuu, Clementine Nkweta-Salami, na kumuhakikishia ushirikiano zaidi kati ya Wizara yake na Shirika hilo.
Mazungumzo hayo ya zaidi ya saa moja yalifanyika ofisini kwa Mhandisi Masauni, jijini Dodoma, leo ambayo yalijadili masuala mbalimbali ikiwemo uimarishaji wa ushirikiano hasa katika kuhakikisha wakimbizi wanalindwa na kuhudumiwa ipasavyo.
Naibu Waziri Masauni alimuhakikishia Mkurugenzi huyo Tanzania itaendelea kulinda haki za wakimbizi kama ilivyokuwa kwa miaka mingi, na pia inasimamia zoezi la kuwarejesha kwa hiari nchini kwao Wakimbizi kutoka Burundi.
“Nikuhakikishie tu, Serikali ya Tanzania inawajali wakimbizi, ndio maana kwa miaka mingi inaendelea kuwahifadhi, hivyo katika kipindi hiki cha kuwarejesha nchini kwao tunahakikisha wanarudishwa wakimbizi wote kwa hiari,” alisema Masauni.
Aidha, Masauni alisema mazungumzo zaidi kuhusu wakimbizi waliopo nchini yatajadiliwa zaidi na kukubaliana katika mkutano wa pande tatu unaotarajiwa kufanyika hivi karibuni.
Naibu Waziri alimshukuru Mkurugenzi huyo ambaye aliambatana na Mwakilishi Mkazi wa Shirika hilo hapa nchini, Chansa Kapaya.