Home Mchanganyiko DKT. KIJAJI: WATANZANIA WAFUNGUE KAMPUNI ZA BIMAKUONGEZA USHINDANI

DKT. KIJAJI: WATANZANIA WAFUNGUE KAMPUNI ZA BIMAKUONGEZA USHINDANI

0

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb), akieleza kuongezeka kwa  wigo na fursa za upatikaji wa huduma za fedha kwa wananchi utakao tokana na  Mpango Mkuu wa Taifa wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha kwa kipindi cha miaka 10 kuanzia mwaka 2019/2020 hadi 2029/2030, katika Kikao  kilichofanyika Jijini Dodoma.

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji, akifungua kikao cha kujadili rasimu ya Mpango Mkuu wa Taifa wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha kwa kipindi cha kuanzia mwaka 2019/2020 hadi 2029/2030, kushoto ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Adlof Ndunguru, na kulia ni Mchumi Mkuu wa Wizara hiyo Bi. Dionisia Mjema.

Baadhi ya wadau wa Kikao cha kujadili rasimu ya Mpango Mkuu wa Taifa wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha kwa kipindi cha kuanzia mwaka 2019/2020 hadi 2029/2030, wakifuatilia kwa makini maagizo ya Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) (hayupo pichani) kuhusu Sekta ya Fedha kuchangia katika uchumi wa nchi.

Mchumi Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Bi. Dionisia Mjema, akitoa mada katika Kikao cha kujadili rasimu ya Mpango Mkuu wa Taifa wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha kwa kipindi cha kuanzia mwaka 2019/2020 hadi 2029/2030, uliofanyika Jijini Dodoma.

Wadau kutoka Wizara ya Fedha na Mipango wakifuatilia majadiliano ya uboreshaji wa rasimu ya Mpango Mkuu wa Taifa wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha kwa kipindi cha mwaka 2019/2020 hadi 2029/2030, uliofanyika Jijini Dodoma.

Wadau wa Kikao cha kujadili rasimu ya Mpango Mkuu wa Taifa wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha kwa kipindi cha kuanzia mwaka 2019/2020 hadi 2029/2030, wakifuatilia mada iliyokuwa ikitolewa na Mchumi Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Bi. Dionisia Mjema.

(Picha na Peter Haule, WFM, Dodoma)

…………………….

Na Peter Haule na Ramadhani Kissimba, WFM, Dodoma

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Ashatu Kijaji amewataka watanzania ambao wamepata elimu ya Bima kufungua Kampuni za Bima za ndani ili ziweze kuingia katika ushindani na kampuni za nje.

Rai hiyo imetolewa wakati wa ufunguzi wa kikao cha wadau cha kujadili na kutoa maoni kuhusu rasimu ya Mpango Mkuu wa Taifa wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha kwa kipindi cha miaka 10 kuanzia mwaka 2019/2020 hadi 2029/2030.

Dkt. Kijaji amesema kuwa, kampuni za bima nchini ni takribani 31 na kati ya hizo za kitanzania hazidi tatu, kwa hiyo kuna  kazi kubwa ya kufanya ili vijana waliopata elimu kwenye eneo la Bima waweze kuanzisha kampuni za kitanzania  na kuwa na ushindani iwapo kama Taifa limeamua kwenda  kwa pamoja.

 

Aidha alisema kuwa,  kuna taasisi za huduma ndogo za fedha takribani 450 lakini jambo la kushangaza ni asilimia 12 tu ya wakina mama ndio wamefikiwa na taasisi hizo hivyo kikao kazi cha kujadili Mpango Mkuu wa Taifa wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha kwa kipindi cha miaka 10 kuanzia mwaka 2019/2020 hadi 2029/2030 utangalia njia mwafaka ya kutatua tatizo hilo.

Alisema kuwa Serikali imeendelea kutekeleza Mpango wa Pili wa Maendeleo wa miaka mitano ambao ulianza mwaka 2016/17 na unaelekea kukamilisha mwaka 2020/21, dhima kuu ilikuwa ni kujenga uchumi wa Viwanda ili kuchochea mageuzi ya kiuchumi na maendeleo ya watu.

“Dhima ya Mpango huu ni uchumi wa Viwanda lakini tusiwaache watanzania nje ya uchumi huu na miongoni  mwa vipaumbele ni kuondoa umasikini wa kipato kwa watu, uimara wa sekta ya fedha ndio nyenzo muhimu ya uimara wa Sekta ya viwanda”, alieleza Dkt. Kijaji.

Alisema kuwa kwa kutambua umuhimu wa sekta ya fedha katika kukuza uchumi na kupunguza umaskini, Serikali inandaa Mpango Mkuu wa Taifa wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha ambao utatumika kuongeza upatikanaji wa huduma jumuishi za fedha, upatikanaji wa mitaji ya muda mrefu, kulinda watumiaji wa huduma za fedha na  kuimarisha uthabiti wa sekta ya fedha

 

Naibu Waziri Dkt. Kijaji, amewataka wadau wa kikao cha uboreshaji wa  rasimu ya Mpango Sekta Ndogo ya Fedha kujadili na kutoa maoni kwa weledi wa hali ya juu yatakayo saidia kuwa na sekta ya fedha iliyo endelevu na himilivu kwa ukuaji wa shughuli za kiuchumi na kuchangia kupunguza umaskini wa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla

 

Kwa upande wake Mchumi Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Bi. Dionesia Mjema, alisema kuwa maagizo yote yaliyotolewa na Naibu Waziri Dkt. Ashatu Kijaji yatafanyiwa kazi na makundi ya wadau waliopo wakiwemo wa Benki, huduma za Bima na kundi litakalo angalia Sekta ndogo ya fedha, lengo ni kuangalia namna ya kutatua changamoto za Sekta ya Fedha kwa kipindi cha miaka kumi ijayo.