Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na
Utawala Bora, Kapt. (Mst), Mhe. George H. Mkuchika (Mb) akizungumza
na wananchi na wadau (Hawapo pichani) waliohudhuria uzinduzi wa
Kampeni ya UTATU ya kupambana na rushwa ya barabarani inayohusisha
TAKUKURU, Jeshi la Polisi na Wadau mbalimbali, uliofanyika jana katika
Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam.
Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na
Utawala Bora, Dkt. Francis Michael akitoa neno la utangulizi kuhusu
uzinduzi wa Kampeni ya UTATU ya kupambana na rushwa ya barabarani
kabla ya kumaribisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya
Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt. (Mst), Mhe. George H.
Mkuchika (Mb) kuzindua rasmi kampeni hiyo kwa niaba Waziri Mkuu wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa (Mb) katika
Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam jana.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na
Utawala Bora, Kapt. (Mst), Mhe. George H. Mkuchika (Mb) akikata utepe
kuzindua rasmi Kampeni ya UTATU ya kupambana na rushwa ya
barabarani inayohusisha TAKUKURU, Jeshi la Polisi na Wadau
mbalimbali, uzinduzi huo uliofanyika jana katika Viwanja vya Mnazi
Mmoja jijini Dar es Salaam.Mkurugenzi wa Kuzuia Rushwa wa TAKUKURU Bi. Sabina Seja
akizungumza kwa niaba Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU kuhusu
uzinduzi wa Kampeni ya UTATU ya kupambana na rushwa ya barabarani
inayohusisha TAKUKURU, Jeshi la Polisi na Wadau mbalimbali ulifanyika
jana katika Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam jana.
*******************************
Na James K. Mwanamyoto-Dar es Salaam
Novemba 02, 2019
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) na Jeshi la Polisi
nchini zimetakiwa kufanyia kazi taarifa za rushwa zinazotolewa na wananchi na
wadau ili kuwajengea imani kuendelea kutoa taarifa za vitendo vya rushwa
zitakazowezesha vyombo hivyo kuendeleza mapambano dhidi ya rushwa
barabarani kwani kumekuwa na malalamiko ya uwepo wa rushwa hiyo.
Wito huo umetolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi
wa Umma na Utawala Bora, Kapt. (Mst), Mhe. George H. Mkuchika (Mb) kwa
niaba ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim
Majaliwa (Mb) wakati akizindua Kampeni ya UTATU ya kupambana na rushwa
ya barabarani na Mfumo wa Kuchukua Taarifa (TAKUKURU Mobile App)
inayohusisha TAKUKURU, Jeshi la Polisi na Wadau mbalimbali ili kuhakikisha
kunakuwa na usalama barabarani na hatimaye kupunguza ajali za barabarani.
Mhe. Mkuchika amewataka wananchi kutenda haki kwa kutoa taarifa za ukweli
zinazojitosheleza na kuongeza kuwa fursa hii isitumike kuwakomoa wasimamizi
wa Sheria za Barabarani ambao kwa namna moja au nyingine tumekwaruzana
nao katika shughuli zetu za kila siku.
Pia, Mhe Mkuchika ametoa wito kwa wadau kushiriki kikamilifu katika kampeni hii
na kumtaka kila mdau kutoa taarifa ya vitendo vya rushwa atakavyokutana navyo
pindi anapotumia barabara.
“Serikali inamtaka kila mdau kujenga tabia ya kuhoji na kutoa taarifa pale
ambapo mazingira yanaonyesha au kuashiria uwepo wa rushwa barabarani na
kwa kufanya hivyo tutakuwa na uzalendo kwa nchi yetu”, Mhe.Mkuchika
amehimiza.
Kabla ya Kumkaribisha Mhe. Mkuchika kuzindua Kampeni ya UTATU, Naibu
Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora,
Dkt. Francis Michael amesema vitendo vya rushwa vinavyofanywa na baadhi ya
watumiaji wa barabara vinachafua taswira ya nchi na kupunguza sifa tunazopata
katika vita dhidi ya rushwa, hivyo kunahitajika ushirikiano wa dhati wa wadau
wote ili kupambana kikamilifu katika vita hii ya rushwa barabarani.
Dkt. Michael amesema siku hii ya Uzinduzi wa Kampeni ya UTATU ni maalum
katika kuhakikisha wadau wanashiriki kikamilifu kusimamia utekelezwaji usalama
wa barabarani na ndio maana Serikali itazindua mfumo rasmi wa TAKUKURU
Mobile App utakaowezesha wananchi kutoa taarifa za vitendo vya rushwa
barabarani ili kuepusha ajali zinazosababishwa na vitendo vya rushwa.
Awali, Mkurugenzi wa Kuzuia Rushwa wa TAKUKURU Bi. Sabina Seja
akimuwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU amesema, lengo la kujumuika
pamoja ni kuendeleza msukumo katika mapambano dhidi ya Rushwa pamoja na
kupata nafasi ya kuielimisha na kuishirikisha jamii kuhusu tatizo la vitendo vya
rushwa barabarani ambalo tafiti nyingi zilizofanyika zinaonesha kuwa wananchi
wanalalamikia vitendo hivyo.
Bi. Seja amesema, Kampeni inayohusu UTATU itawawezesha wadau kutafakari
kwa pamoja hatua zinazopaswa kuchukuliwa kukabiliana na tatizo la rushwa
barabarani.
Bi. Seja ameyataja malengo ya Kampeni ya UTATU kuwa, ni kudhibiti vitendo
vya rushwa miongoni mwa wasimamizi wa sheria za barabarani, kuandaa
mkakati wa kuzuia vitendo vya rushwa barabarani, kushirikisha umma kuzuia
vitendo vya rushwa barabarani na kutumia TEHAMA kudhibiti vitendo vya
rushwa barabarani ambapo tayari TAKUKURU imeshatengeneza mfumo wa
TAKUKURU App ambao utakaowawezesha wananchi kuchukua matukio ya
vitendo vya rushwa kwa kutumia simu za mkononi kupiga picha za video, mnato
na kurekodi sauti na kutuma katika mfumo huo ili kufanyiwa kazi.
Naye, Inspekta Jenerali wa Jeshi la Polisi nchini (IGP) Simon Sirro amesema
mkakati wa Kampeni ya UTATU ni sehemu ya matakwa ya kihistoria na kitaasisi
katika jitihada za kupambana na rushwa chini ya Sheria ya Kuzuia na
Kupambana na Rushwa Na. 11 ya Mwaka 2007 ambayo ilitungwa baada ya
kufutwa Sheria ya Kuzuia Rushwa ya TAKUKURU Sura 329 iliyofanyiwa marejeo
mwaka 2002.
Kauli mbiu ya Kampeni hii UTATU iliyozinduliwa na Serikali kwa Ushirikiano wa
TAKUKURU, Jeshi la Polisi na wadau mbalimbali inasema ‘KWA USALAMA
WAKO KATAA RUSHWA BARABARANI’.