Home Mchanganyiko Wakala wa Chakula na Dawa Zanzibar (ZFDA) wameangamiza bidhaa mbali mbali.huko jaa...

Wakala wa Chakula na Dawa Zanzibar (ZFDA) wameangamiza bidhaa mbali mbali.huko jaa la kibele

0

 Mfanya Biashara wa Bidhaa ya Mchele ulioangamizwa tani 105 kutoka Kampuni ya Ahmed Khelef, Ibrahim Omar Awesu akitoa maelezo kuhusu kuharibika kwa bidhaa hiyo  huko Jaa la Kibele Mkoa wa Kusini Unguja.

Mkuu wa Kitengo cha Uchambuzi wa athari zitokanazo na Chakula kutoka Wakala wa Chakula na Dawa Zanzibar (ZFDA) Aisha Suleiman akitoa maelezo kuhusu bidhaa mbali mbali za Chakula tani 133.5 zilizoharibika na kuangamizwa huko Jaa la Kibele Mkoa wa Kusini Unguja.

Wafanyakazi kutoka  Wakala wa Chakula na Dawa Zanzibar (ZFDA) wakiangamiza bidhaa mbali mbali za Chakula na Vipodozi katika  Jaa la Kibele Mkoa wa Kusini Unguja.

Picha na Maryam Kidiko – Habari Maelezo Zanzibar.

******************************

Na Miza Kona Maelezo Zanzibar 02/11/2019

Wakala wa Chakula, Dawa na Vipodozi Zanzibar (ZFDA)  imeteketeza zaidi ya tani 130 za bidhaa za chakula na tani tano za vipodozi zilizoharibika katika jaa la Kibele wilaya ya Kusini Mkoa wa Kusini Unguja.

Akizungumza na waandishi wa habari Mkuu wa Kitengo cha  uchambuzi wa Athari zitokanazo na Chakula wa ZFDA Aisha Suleiman amesema bidhaa hizo zilikaguliwa na kuonekana hazifai kwa matumizi ya binadamu.

Alisema kuwa bidhaa hizo ambazo baadhi yake zikiwa zimeharibika na nyengine zikiwa zimeingia nchini bila kufuata utaratibu wa uingizaji bidhaa zilikamatwa katika maeneo mbalimbali ya Zanzibar.

Alizitaja bidhaa zilizoangamizwa kuwa ni mchele tani 105 ulioingizwa na  kampuni ya Ahmed Khelef, majani ya chai tani 24 kutoka kampuni ZATEPA, bidhaa mchanganyiko tani moja, pipi tani moja na nusu kutoka kampuni Basil Cook pamoja na soda za kopo tani mbili kutoka kampuni ya Ahmed Salim.

Amefahamisha bidhaa zinazoingia nchini zinatakiwa kufuata taratibu zote za uingizaji ikiwa pamoja na kufanyiwa ukaguzi na maafisa wa Wakala wa Chakula na Dawa ili kuhakikisha kuwa bidhaa hizo zipo salama na hazina madhara kwa mtumiaji.

Aidha Mkuu huyo amewataka wafanya biashara na wananchi kuwa waangalifu wakati wanapnunua na kusafirisha bidhaa ili kuhakikisha zinaingia nchini zikiwa bado hazijaharibika.

Kaimu Mkurugenzi Idara ya Dawa na Vipodozi wa ZFDA Nassir Buheti amesema vipodozi vilivyotekezwa baadhi yake vina sumu ambayo ni hatari kwa afya ya binadamu.

Amefahamisha kuwa vipodozi hivyo vimeingia nchini kinyume na utaratibu  havijaisha muda wake wa matumizi bali vimeonekana kuwa vinaviambato  vyenye sumu havipo salama kwa mtumiaji.

Kwa upande wake Mfanyabiashara Ibrahim Omar Awesu kutoka Kampuni ya Ahmed Khelef alisema walinunua mchele huo ukiwa katika hali nzuri kwa matumizi lakini uliharibika kutokana na kampuni ya usafirishaji kuchelewa kuusafirisha na kusababisha na hatimae kuharibika ukiwa njiani kuja Zanzibar.

Aidha ameomba wakala wa Chakula wa Dawa kufanya mapema ukaguzi wa bidhaa zinazoingia nchini pamoja na makampuni ya usafirishaji kuingiza bidhaa hizo kwa wakati ili kuepuka hasara.