Dar es Salaam. Waogeleaji wa timu ya Taifa ya Tanzania waliochaguliwa kuunda timu ya Taifa kwa ajili ya mashindano ya dunia wapo katika hatihati ya kushiriki kutokana na ukata wa Chama Cha Kuogelea Tanzania (TSA).
Tanzania imepata nafasi ya kushiriki katika mashindano mawili, mashindano ya dunia ya waogeleaji wakubwa yaliyopangwa kufanyika Gwangju, Korea Kusini kuanzia Julai 12 mpaka 28 na mashindano ya vijana yaliyopangwa kufanyika Budapest, Hungary kuanzia Agosti 20 mpaka 25.
TSA imewachaguwa waogeleaji wanne, Hilal Hilal, Collins Saliboko (wanaume) na wanawake ni Sylvia Caloiaro na Shivani Bhatt. Waogeleaji hao wataambatana na kocha wao, Alexander Mwaipasi na viongozi wawili, Mwenyekiti, Imani Alimanya na makamu wake, Asmah Hilal.
Chama hicho kinahitaji Sh38,772,000 kwa ajili ya mashindano hayo huku shirikisho la dunia la mchezo huo, Fina litagharimia ticketi za safari tu kwa waogeleaji watatu na viongozi wawili kwa masharti ambayo yanaitaka TSA kutumia gharama zake na baadaye kurudishiwa mara baada ya mashindano.
Fina pia imeitaka TSA kutafuta Sh80,760,000 kwa ajili ya kuwasafirisha waogeleaji saba kwa ajili ya mashindano ya dunia ya vijana. Waogeleaji hao ni Dennis Mhini, Delvin Barick, Christopher Fitzpatrick, Christian Shirima na Isam Sepetuambao watashindana kwa upande wa wavulaa na wasichana, Kayla Temba na Laila Rashid.
Kama ilivyo kwa waogeleaji wakubwa, Fina italipia waogeleaji watatu na kiongozi mmoja tu kwa masharti kuwa shirikisho la dunia litarejesha fedha hizo mara baada ta TSA kuwasilisha madai mara baada ya mashindano.
Katibu Mkuu wa TSA, Inviolata Itatiro alisema kuwa masharti hayo yanawafanya wao (TSA) kutafuta Sh milioni 120, jambo ambalo linawaweka katika wakati mgumu.
“Tunawaomba wadau watusaidie kupata fedha hizo. Shirikisho letu halina fedha na kwa sasa tupo katika hatihati ya kushiriki kutokana na hali hiyo,” alisema Inviolata.
Alisema kuwa hata waogeleaji ambao wapo chini ya Fina, hawataweza kwenda kushindana kama hatutaweza kutafuta fedha ambazo baadaye Fina watarejesha.
“Tupo katika wakati mgumu sana, tunaomba wadau na serikali itusaidie, waogeleaji wetu wapo katika mazoezi makali na wana nia ya kufanya vizuri katika mashindano hayo,” alisema.