Home Mchanganyiko SERIKALI INAJENGA NYUMBA ZA GHARAMA NAFUU ILI KUWAWEZESHA WATUMISHI WA UMMA KUPATA...

SERIKALI INAJENGA NYUMBA ZA GHARAMA NAFUU ILI KUWAWEZESHA WATUMISHI WA UMMA KUPATA MAKAZI BORA

0

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb)  akihimiza uwajibikaji kwa watendaji wa Watumishi Housing Company (hawapo pichani) kabla ya kutembelea miradi ya ujenzi wa nyumba za makazi  ya Watumishi wa Umma  zilizopo Gezaulole Kigamboni na Bunju B mkoani Dar es Salaam.

Mkurugenzi Mtendaji wa Watumishi Housing Company, Dkt. Fred Msemwa akiwasilisha kwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) taarifa ya utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa nyumba za makazi  ya Watumishi wa Umma  zilizopo Gezaulole Kigamboni.

Mwonekano wa baadhi ya majengo ambayo ni nyumba zilizojengwa  na Watumishi Housing Company kwa ajili ya makazi kwa Watumishi wa Umma na Wanachama wa Mifuko ya Hifadhi za Jamii kwa lengo la kuwauzia na kupangisha.

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb)  akikagua baadhi ya nyumba  za makazi  zilizojengwa  Bunju B mkoani Dar es Salaam kwa ajili ya kuuza na kuwapangisha Watumishi wa Umma na Wanachama wa Mifuko ya Hifadhi za Jamii.

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) akitoa maelekezo kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Watumishi Housing Company, Dkt. Fred Msemwa mara baada ya kutembelea miradi ya ujenzi wa nyumba za makazi  ya Watumishi wa Umma  na Wanachama wa Mifuko ya Hifadhi za Jamii zilizopo Gezaulole Kigamboni na Bunju B mkoani Dar es Salaam.

…………………

Serikali imeendelea kuwajali Watumishi wa Umma nchini kwa kuwajengea nyumba bora za gharama nafuu kupitia miradi ya ujenzi wa nyumba inayotekelezwa na Watumishi Housing Company katika maeneo mbalimbali nchini ili kuwawezesha watumishi kumiliki nyumba bora za kuishi.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) alipotembelea miradi ya ujenzi wa nyumba za makazi Gezaulole Kigamboni na Bunju B mkoani Dar es Salaam.

Mhe. Dkt. Mwanjelwa amesema, amejionea nyumba zilizojengwa kisasa, gharama nafuu na zenye viwango vinavyostahili kwa makazi ya watumishi wa umma na wanachama wa mifuko ya hifadhi ya jamii ambao ndio walengwa wakuu wa miradi hiyo.

Aidha, Mhe. Dkt. Mwanjelwa amewaagiza watendaji wa Watumishi Housing Company kuhakikisha wanakuwa na mkakati madhubuti wa kutoa taarifa kwa watumishi wa umma juu ya uwepo wa nyumba zilizojengwa na kampuni hiyo, sehemu zilipo na bei elekezi kwa wanaohitaji kununua, ikiwa ni pamoja na bei ya kupangisha.

Mhe. Dkt. Mwanjelwa amekamilisha ziara yake ya kikazi mkoani Dar es Salaam ya kukagua miradi ya ujenzi wa nyumba za makazi ya Watumishi wa Umma na  wanachama wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii na kuhimiza uwajibikaji kwa watendaji wa Watumishi Housing Company.