Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) akizungumza na vyombo vya habari katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya Ushirika Duniani yaliyofanyika mkoani Tabora mwishoni mwa wiki.
Waziri wa Kilimo Hussein Bashe akisalimiana na Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania alipotembelea banda la Mamlaka wakati wa kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Ushirika Duniani yaliyofanyika mkoani Tabora mwishoni mwa wiki.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Christina Mndeme (wa kwanza kushoto) akifuatilia kwa makini hotuba ya Waziri wa Kilimo Hussein Bashe wakati wa kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Ushirika Duniani yaliyofanyika tarehe 01 .07 . 2023 mkoani Tabora.
Washiriki wa Maadhimisho ya Siku ya Ushirika Duniani 2023 wakimsikiliza Waziri wa Kilimo Hussein Bashe wakati wa kilele cha maadhimisho hayo.
……………………….
Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) imetoa mafunzo kwa vyama vya ushirika 404 ambavyo vitakuwa mawakala wa kusambaza mbolea nchini katika msimu wa kilimo wa 2023/2024.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania Dkt. Stephan Ngailo ameyasema hayo jana tarehe 1.07.2023 mkoani Tabora alipozungumza na vyombo vya habari
wakati wa kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Ushirika Duniani,
yanayofanyika kuanzia tarehe 26 Juni hadi tarehe 1.07 kila mwaka.
Dkt.Ngailo amesema hadi kufikia tarehe 30 Juni 2023 Mamlaka imekwisha kusajili vyama vya ushirika 285 vitakavyounganishwa na makampuni ya mbolea ili kusambaza mbolea za ruzuku kwa wakulima katika maeneo mbalimbali nchini.
Dkt. Ngailo amebainisha kuwa vyama hivyo vya ushirika vinategemewa kuwa suluhisho la usambazaji wa mbolea kwani vitasogeza huduma hiyo karibu zaidi na wakulima tofauti na msimu uliopita wa 2023/2024.
Akizungumza mapema wakati wa kufunga Wiki ya Ushirika Waziri wa Kilimo Hussein Bashe amesema serikali itaendelea kutoa ruzuku ya mbolea kwa wakati na tayari Kampuni ya Mbolea ya Taifa (TFC) imepatiwa kiasi cha Dola milioni 71 na wamekwisha agiza mbolea hiyo.
Waziri Bashe amesema ruzuku pia itatolewa katika viwanda vya ndani ili vizalishe mbolea ya kutosha na kuuza kwa bei nafuu.
Aidha Waziri Bashe amesema serikali itapima afya ya udongo nchi nzima ili kujua aina za udongo na mazao yanayofaa kulimwa kila eneo.
Ameongeza kuwa maelekezo ya Mhe.Rais Samia ni kuongeza matumizi ya mbolea kutoka kilo 19 kwa hekta za sasa hadi kufikia kilo 50 ifikapo mwaka 2030.