Wakati zoezi la fidia ya Majengo, Mashamba na Viwanja likiendelea ili kupisha Ujenzi wa Reli ya kisasa – SGR Morogoro – Makutupora, Shirika la Reli Tanzania – TRC linaendelea kuhamasisha wananchi kushiriki zoezi la Kuhamisha Makaburi linaloendelea mkoani Dodoma hivi karibuni Oktoba 2019.
Zoezi la uhamasishaji wa makaburi yapatayo zaidi ya 600 linahusisha, viongozi wa wilaya, serikali za vijiji, wataalamu wa afya toka serikalini, watendaji na maafisa wa shirika la reli TRC.
Katika awamu hii, vijiji vipatavyo sita vilivyopo wilayani Dodoma vitahusika na zoezi hili, Vijiji hivyo ni pamoja na Ihumwa, Makulu, Tambuka Reli, Kilimani, Kikuyu Kusini, Mkonza, Bwawani, Muungano na Zuzu.
Katika zoezi hilo wananchi wameonesha kuridhika na utendaji wa serikali ya awamu ya tano inayoongozwa Rais John Pombe Magufuli kwa kuridhia makaburi yao kuhamishwa ili ujenzi uendelee.
Kikosi cha wataalam wa masuala ya kijamii kutoka TRC kimefanya kazi ya kutoa elimu na kuhamasisha wananchi ambao maeneo yao yakiwemo Makaburi ya wapendwa wao yamepitiwa na mradi kuunga mkono jitihada za Mhe. Rais Magufuli kwa kushiriki kikamilifu katika Mradi wa SGR
Akihamasisha wananchi wa Kijiji cha Makulu Afisa wa Masuala ya Kijamii kutoka TRC Bwana Leodgard Lazarus aliwafahamisha wananchi juu ya changamoto ya kutoa kifuta machozi kabla ya kuhamisha makaburi kwamba baadhi ya wahusika wakishalipwa fedha hizo hawarudi kwa ajili ya kuhakiki makaburi.
Aidha aliongeza kuwa wahusika wasiporudi kwa ajili ya uhakika inakuwa ngumu Shirika kuweka ripoti za uhamishaji makaburi kwa ajili ya kupisha Ujenzi wa Reli ya kisasa.
Shirika linaendelea na kazi kubwa ya Usimamizi wa Mradi wa Ujenzi wa Reli ya kisasa kuanzia Dar es Salaam – Makutupora mkoani Singida ambapo kwa kushirikiana na Serikali za Mikoa, Wilaya, na Mitaa ambayo reli ya kisasa inapita wananchi wameendelea kulipwa fidia na vifuta machozi ila kupisha mradi uendelee na ukamilike kwa wakati