Na Mwandishi Wetu, Katavi
RAIS Dk. John Pombe Magufuli amewafuta machozi wafugaji wa Tanzania baada ya kuamuru wananchi waliokuwa wakiishi katika vijiji 920 vilivyokuwa ndani ya Hifadhi kutoondolewa na kuendelea shughuli zao za ufugaji na kilimo na kuondokana na kadhia ya kukamatwa , kuchomewa nyumba zao na kupigwa faini kubwa kila siku na Maafisa wa Wizara ya Maliasili na Utalii.
Akizungumza kwa nyakati tofauti katika ziara yake inayoendelea Mikoa ya Rukwa na Katavi, Rais Magufuli amesema kwa miaka mingi wafugaji Tanzania wamekuwa wakiishi kwa manyanyaso makubwa jambo ambalo Serikali anayoiongoza kamwe haitakubali liendelee.
Rais Magufuli amesema asilimia 32.5 ya nchi ya Tanzania ni hifadhi huku idadi ya wananchi na shughuli za ufugaji na kilimo zikiendelea kuongezeka siku hadi siku na kutumia eneo lilibaki la asilimia 68 tu huku maeneo mengine ya nchi yakiwa ni mito, maziwa hivyo eneo lililokuwa limebaki kwa ajili ya matumizi ya binadamu lilikuwa dogo na ndio maana kumekuwepo na migogoro baina ya wafugaji, wakulima na watumiaji wengine wa ardhi.
“Mtu ukienda kwenye shamba fulani umevamiwa, wananyanyaswa wananchi saa nyingine na kupigwa faini za ajabu ajabu umeingiza ng’ombe zako kuchunga zinashikwa..unataka ukachungie wapi ng’ombe wanaoshika ..nyama wanataka na maziwa wanataka lakini ng’ombe wanakupiga faini imekuwa ni nchi yenye migogoro”alisema Rais Magufuli.
Pia Rais Magufuli akabainisha kuwa watu waliopewa dhamana ya uongozi kwa bahati mbaya hawakutumia nafasi zao kutafuta suluhu ya migogoro hiyo badala yake wakawa wanatumia nguvu katika kutatua na kusababisha manyanyaso makubwa kwa wananchi .
“Bahati mbaya sisi hatukutumika kama njia mbadala ya kutatua migogoro tukawa tunatumia nguvu katika kutatua migogoro tunaenda porini mle tunawafyeka watu kwa kuchoma mazao yao wakinamama wanalia hawa ni watanzania ni wazalishaji wazuri ni wafugaji na wakulima hapakuwa na sababu ya kuwa tunaenda tunawafukuza kila mahali kwa sababu….sababu za msingi zingine zipo kwamba ardhi haitoshi”alisema Rais Magufuli.
Dk. Magufuli akafafanua kuwa ndio maana ilimlazimu kuunda timu ya mawaziri 8 kwani aliapa kuwatumikia watanzania masikini wakiwemo hata hao waliovamia maeneo na kamwe hatokubali watu waonewe na kusisitiza kuwa timu hiyo ya mawaziri imefanya kazi nzuri sana kwa kuzngukia maeneo mbalimbali nchini yaliyokuwa na migogoro wakaja na mapendezo vijiji 920 vilivyokuwa ndani ya hifadhi tukaamua vibaki.
“Tukaamua vijiji vibaki humo wala wasiondolewe humo, tukaamua mapori tengefu 12 tuyafute, misitu ya hifadhi 7 iliyokuwa imepoteza sifa zibaki kwa wananchi kwa ajili ya shughuli za makazi , kilimo na mifugo tukaamua kumega hifadhi za misitu 14 kwa ajili ya kilimo na kufuta mashamba 16 ambayo yalikuwa hayaendelezwi na hayo ndio yalikuwa maelekezo yangu”alisema Rais Magufuli.
Hivyo wananchi wa vijiji hivyo wataendelea kuishi humo na sio hifadhi tena na kuwaonya watu wa hifadhi waliokuwa waenda kuwasumbua wananchi wasisogee kabisa katika vijiji hivyo na kusisitiza kuwa uamuzi huo umefanywa kwa kutambua shida za wananchi.
Pia ameonya kuwa uamuzi uliofanywa na Serikali wa kuvibakiza vijiji hivyo isiwe chanzo cha wananchi kuvamia tena hifadhi na kutaka kuongezewa vijiji vipya kwa Serikali yake haitaongeza tena kijiji kingine.
“Msije mkasema na huku tukivamia tutaachiwa mkivamia utatolewa kwa nguvu , utatolewa kwa kuvamiwa hivyo hivyo ni lazima tusemezane ukweli, msema kweli ni mpenzi wa Mungu ..uongozi wa Mkoa na Wizara ya Ardhi ikapange vizuri matumizi ya ardhi ili isiwe sababu tena ya kwenda kugombanisha watu wale watu wenye maeneo yao waendelee kubaki na maeneo yao kama alikuwa na eneo kubwa basi ni bahati yake imemkuta huko asitokee tena mtu alikuwa na ekari 20 ukampunguzia akawa na ekari 5 hapana aliyewahi kawahi, aliyechelewa shauri yake”alisema Dk. Magufuli
Hivyo aliwataka wananchi walionufaika na ardhi hiyo kuitumia vizuri kwa ajili ya shughuli za uzalishaji wa mifugo na kilimo ili waweze kupata manufaa makubwa na kutajirika kwani Serikali ya awamu ya tano sio ya kutesa watu.
‘Mkatajirike ndugu zangu huu ndio wakati wa kutajirika, awamu hii ya tano si awamu ya kutesa watu ni awamu ya kuwatajirisha watu”alisisitiza Rais Magufuli.
Kwa upande wake Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina alimshukuru Rais Magufuli kwa kuwa kiongozi pekee wa Tanzania aliyekubali kutatua migogoro ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi na kumhakikishia kuwa kazi ya kulinda soko la ndani la bidhaa za mifugo na uvuvi inafanyika vizuri na kwamba mianya yote imezibwa na makufuli na hakuna tena mtu atakayechezea soko la Tanzania.
Waziri Mpina amesema pia wafugaji wengi wa mikoa ya Rukwa na Katavi wamekuwa wakiteseka kwa kukosa soko la mifugo yao kutokana na kiwanda cha SAAFI kilichopo mkoani Rukwa kutofanya kazi ipasavyo na kumthibitishia Rais Magufuli kuwa Serikali itafanya jitihada zote kuhakikishia kiwanda hicho kinafanya kazi vizuri ili wafugaji wa mikoa hiyo wapate soko la uhakika la mifugo yao.