Wamiliki wa Kampuni ya Kufua Umeme ya IPTL, Habinder Sethi na James Buchard Rugemalira, wameandika barua kwa Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), kuomba msamaha na kukiri mashitaka ya uhujumu uchumi yanayowakabili mahakamani hapo.
Hata hivyo imebainika kuwa, Seth aliandika barua yake hiyo iliyopitia kwa mkuu Wa Gereza Mapema Mwezi huu baada msamaha huo kutangazwa na Rais Dk John Magufuli ambae alimuelekeza DPP kuwa washtakiwa wenye mashtaka ya uhujumu uchumi ambao wako tayari kukiri makosa yao waandike barua ya kuomba msamaha ili kurejesha hasara waliyosababisha.
Mapema leo asubuhi Oktoba 10,2019 Wakili Michael Ngaro anayemtetea Rugemalira amedai kuwa mteja wake ameandika barua kwa DPP kuomba kukiri makosa ya uhujumu uchumi yanayomkabili na kwamba mpaka sasa hawajapata majibu.
Washtakiwa hao ambao kwa mara ya kwanza walifikishwa mahakamani hapo Juni 19, 2017.
wanakabiliwa na mashitaka 12 yakiwemo ya utakatishaji fedha na kusababisha hasara ya USD 22,198,544.60 na Sh 309,461,300,158.27
Kufuatia taarifa hiyo Ngaro ameuomba upande wa mashitaka kufanya mchakato ili wapate majibu ya barua hiyo haraka
Akijibu hoja hiyo, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon amedai kuwa, ni kweli wamepokea barua za washtakiwa wote wawili na kwamba zinafanyiwa kazi na watapatiwa majibu.
Kesi hiyo ambayo leo ilikuja kwa ajili ya kutajwa imeahirishwa hadi Oktoba 24, mwaka huu kwa ajili ya kutajwa tena
Seth na Rugemalira wako gerezani kwa mwaka wa tatu sasa kutokana na upelelezi wa kesi hiyo kutokamilika.
Washitakiwa hao wanadaiwa, kati ya Oktoba 18, 2011 na Machi 19 , 2014 jijini Dar es Salaam walikula njama katika nchi za Afrika Kusini, Kenya na India ili kutenda kosa.
Aidha, katika mashtaka ya kujipatia fedha inadaiwa, kati ya Novemba 28 na 29, 2011 na Januari 23,2014 katika Makao makuu ya Benki ya Stanbic Kinondoni na Benki ya Mkombozi tawi la Mtakatifu Joseph, kwa ulaghai washitakiwa hao walijipatia kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BOT), USD 22,198,544.60 na Sh 309, 461,300,158.27.
Pia washtakiwa wote wanadaiwa kuisababishia serikali hasara ambapo inadaiwa, Novemba 29, 2013 katika Benki ya Stanbic tawi la kati kinondoni, kwa vitendo vyao waliisababishia serikali hasara ya USD 22, 198, 544.60 na Sh 309,461,300,158.27.
Kati ya Novemba 29,2013 na Januari 23, 2014 maeneo tofauti Dar es Salaam kwa pamoja walitenda kosa la kutakatisha fedha kwa kuchukua fedha kutoka BoT ambazo ni USD milioni 22.1 na Sh bilioni 309.4 wakati wakijua fedha hizo ni zao la kujihusisha na genge la uhalifu.