Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akipata maelezo kutoka kwa Mwakilishi wa Wakala wa Misitu Tanzania Kanda ya Kati Bi. Teddy Yoramu juu ukuaji wa miti iliyopandwa katika eneo la Mzakwe jijini Dodoma wakati wa kampeni ya Kuifanya Dodoma ya Kijani.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan akikagua miti iliyopandwa wakati wa kampeni ya kukijanisha Dodoma katika eneo la Mzakwe jijini Dodoma ikiwa sehemu ya ufuatiliaji wa ukuaji wa miti hiyo.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akisalimiana na Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma Bw. Godwin Kunambi wakati wa ziara ya ukaguzi wa miti iliyopandwa wakati wa kampeni ya kukijanisha Dodoma. Wengine katika picha ni Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Bw. Patrobas Katambi na Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Mhandishi Joseph Malongo.
*******************************
Lulu Mussa na Monica Sapanjo.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amesema azma ya kuifanya Dodoma kuwa ya Kijani iko pale pale.
Hayo yamesemwa leo mara baada ya kutembelea shamba la miti lililopo katika eneo la Mzakwe katika Kambi ya Jeshi la Makutupora Jijini Dodoma, ikiwa ni ufuatiliaji wa Kampeni aliyozindua mwaka 2017 ya kuifanya Dodoma kuwa ya kijani.
Makamu wa Rais ameupongeza uongozi wa Kambi ya Jeshi ya Makutupora, Wakala wa Misitu Tanzania na Watendaji wa Ofisi yake kwa kuhakikisha miti iliyopandwa mwezi Desemba 2017 inastawi.
“Vitabu vya dini vinasema Moja kati ya sadaka endelevu ni kupanda miti, miti hii
imekuwa na kustawi kwasababu ya jitihada zenu za kuimwagilia na kuitunza, msikate tamaa, endeleeni na kazi hii njema ambayo matokeo yake yanaonekana ikiwa ni pamoja na kuimarika kwa mifumo ya hali ya hewa ambayo huimarisha shughuli za kilimo na maendeleo ya viwanda.” Alisisitiza Makamu wa Rais
Nae Mkuu wa Kambi ya Jeshi ya Makutupora Luteni Kanali Festo Mbanga amesema kuwa miti 2300 ilipandwa tarehe 21/12/2017 na kati ya hiyo miti 2076 imekuwa na kustawi ikiwa ni sawa na asilimia 90.3 ya miti yote iliyopandwa.
“Katika miti iliyooteshwa awali baadhi haikuota, hivyo tumefanya jitihada za kuirudishia, tumepanda takriban miti 300 ya ziada” alisema Luteni Kanali Mbanga.
Katika hatua nyingine Makamu wa Rais ameagiza Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) kuhakikisha tafiti zinakamilika mapema kutoka katika sampuli ya udongo iliyochukuliwa ili kubaini aina ya miti inayostawi katika eneo hilo na Jiji la Dodoma kwa Ujumla.
Kampeni ya Kukijanisha Dodoma ilizinduliwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania tarehe 21/12/2017 katika eneo la Mzakwe Jijini Dodoma ambapo miti 2300 ilipandwa siku hiyo.