***********************************
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk.
Ali Mohamed Shein amesema serikali imejidhatiti kuendeleza
kwa vitendo Mapinduzi ya Kilimo kwa kuwapa taaluma ya
kilimo bora wakulima, wafugaji na wavuvi, pamoja na
kuendeleza huduma za ugani.
Dk. Shein amesema hayo katika ufunguzi wa Maonesho ya siku
ya chakula Duniani, yaliofanyika katika viwanja vya
Chamanangwe, Mkoa Wa Kaskazini Pemba.
Alisema katika kutekeleza azma hiyo, Serikali itaendelea kutowa
huduma za matrekta na pembejeo mbali mbali za kilimo, kwa
kutoa ruzuku ya asilimia 75 kama ilivyoahidi .
Alisema Serikali inaendelea kuweka mazingira mazuri ya
kibiashara ili kuwawezesha wafanyabiashara kuingiza na kuuza
zana, vifaa na pembejeo za kisasa kwa wakulima kwa urahisi.
Aidha, Dk. Shein alisisitiza haja ya wakulima kulima kwa
kuzingatia matumizi ya mbinu za kisasa za kilimo pamoja na
kufuata maelekezo ya wataalamu.
Alitaka kuwepo matumizi bora ya pembejeo za kilimo, mbolea
pamoja na kuwataka wakulima kuondokana na kilimo cha
mazowea, akibainisha hatua hiyo italiwezeshaTaifa kuongeza mavuno ya mazao ya chakula na biashara na kutoa uhakika wa chakula na lishe bora.
Rais Dk. Shein aliitaka Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na
Uvuvi kuhakikisha inakuwa na mipango na mikakati madhubuti
katika kuwaelimisha, kuwahamasisha na kuwasaidia wananchi ili
kuwa na mwamko wa kutumia teknoljia bora za kilimo katika
mazao mbalimbali.
“Maarifa watakayopata wananchi kupitia maonyesho haya
yatawasidia kupata mbinu mpya za kuongeza uzalishaji katika
kilimo na kuongeza tija”, alisema.
Aidha, alisema kupitia maonyesho hayo, wananchi watapata fursa
ya kuzijua taasisi mbalimbali zinazotoa mikopo kwa wakulima,
wavuvi na wafugaji pamoja na wajasiriamali na hatimae kuweza
kusaidiwa.
Alisema wananchi wataweza kujifunza na kuitumia elimu
watakayoipata ili kuongeza uzalishaji katika shughuli za kilimo,
uvuvi na ufugaji na hivyo kukuza uchumi pamoja na kujiongezea
kipato cha kujikimu.
Akigusia changamoto za ajira zinazowakabili vijana, Dk. Shein
aliisistiza umuhimu wa kutembelea maonesho hayo ili kuona fursa
za kujiajiri zilizopo.
Alisema serikali itaendelea na juhudi za kuwasaidia vijana kupata
mitaji ya kuendesha shughuli zao kupitia mfuko maalum
ulioanzisha hivi karibuni pamoja na Mfuko wa Khalifa Fund wenye
gharama ya Dola za Kimarekani Milioni 10.
Sambamba na hilo, Dk. Shein alisema katika kipindi cha miaka
mitano serikali imetenga Dola Milioni 10 (sawa na shilingi Bilioni 46) kwa lengo hilo hilo la kuwawezesha vijana kujiajiri na kupunguza kutegemea ajira kutoka serikalini.
Katika hatua nyengine, Dk.Shein alisema Serikali imeanzisha
taasisi ya utafiti wa kilimo, mifugo na uvuvi ili kuziwezesha
shughuli hizo kufanyika kisasa zaidi pamoja na kubaini
changamoto zilizopo, hatua iliyokwenda sambamba na
kukiunganisha Chuo cha Kilimo Kizimbani na Chuo Kikuu cha
Taifa cha Zanzibar (SUZA).
Alitowa wito kwa vijana wenye sifa za kujiunga na masomo ya
utaalamu wa kilimo, mifugo na uvuvi kujiunga na na masomo
hayo ili Taifa lipate wataalamu inaowahitaji.
“Naiagiza Wizara ya Kilimo, maliasili. Mifugo na Uvuvi iendelee
kuwaajiri vijana waliokwisha maliza masomo yao ya kitaalamu
wakumbushwe kazi zao sio kukaaa ofisini, bali wawafuate
wakulima huko waliko, kwani ndio namna bora ya kuwatumikia”,
alisema.
Akigusia uendelezaji wa kilimo cha mpunga, Dk. Shein alisema
kuna mafanikio ya kuongezeka kwa mavuno yalioanza kupatikana
na kusema hivi sasa Serikali imejielekeza katika mradi mkubwa
wa ujenzi wa miundombinu ya uwagiliaji maji kupitia mkopo wa
Dola Milioni 50 kutoka Benki ya Exim ya Jamuhuri ya Korea.
Alisema mradi huo utatekelezwa katika mabonde matano
yanayolimwa mpunga, ikiwemo Cheju, Kilombero, Bumbwisudi,
Mkwararani na Mlemele, hatua itkayopanuwa wigo wa kilimo cha
mpunga wa umwagiliaji kutoka ekari 810 hivi sasa na kufikia ekari
2,397.
Alisema kutokana na ongezeko hilo, kuna matarajio makubwa ya
kuongezeka kwa mavuno ya mpunga nchini kutoka wastani wa tani 31,000 za mchele hadi kufikia tani 70,365, hivyo kupunguza matumizi ya fedha za kigeni katika kuagiza bidhaa hiyo.
“Takwimu zinaonyesha Zanzibar kwa mwaka tunatumia wastani
wa shilingi Bilioni 40.5 kununua mchele peke yake, kiwango hiki
kitapungua kwa kiasi kikubwa na hatimaeckuondoka kabisa”,
alisema.
Aidha, aliwataka Wakuu wa Wilaya kote nchini kuongeza kasi ya
mashirkkiano na Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi,
sambamba na kusimamaia ipasavyo maendeleo ya kilimo katika
Wilaya zao.
Alieleza kuwa mafanikio haliofikiwa na kuongezeka uzalishaji
katika sekta ya kilimo, kunatowa matumaini makubwa katika
miaka michache ijayo Zanzibar itajitosheleza kwa chakula, kuwa
na lishe bora na usalama wa chakula.
Alisema lishe bora na usalama wa chakula ni muhimu katika
kuleta ustawi wa jamii na hasa watoto wenye mahitaji maalum
pamoja na wagonjwa.
Dk. Shein aliipongeza Wizara ya kilimo, Maliasili,Mifugo na Uvuvi
pamoja na Wizara ya Elimu na mafunzo ya Amali kwa kuendeleza
mpango wa kutoe elimu ya lishe bora kupitia maskulini,
akibainisha kuwa ni uamuzi wa serikali katika kuimarisha afya za
watoto pamoja na kukabiliana na utapiamlo.
“Natoa wito kwa wananchi kuzingatia haja ya kula chakula chenye
lishe bora kitakachosaidia kuimarisha afya zetu, tuone umuhimu
wa kula vyakula vya asili vinavypapatikana kwa wingi hapa
nchini,ikiwemo matunda na mboga mboga ili tupate lishe bora”,
alisema.
Mapema, Waziri wa Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi, Mmanga
Mjengo Mjawiri, alisema muelekeo wa sekta ya kilimo ni
kuongeza uzalishaji na usarifu wa mazao ili kuongeza tija kama
ilivyoainishwa katika MKUZA pamoja na Ilani ya Chama cha
Mapinduzi ya 2015-2020.
Aliipongeza serikali kwa juhudi za kutoa kipaumbele katika sekta
ya kilimo, ili kuona uzalishaji wa chakula onaongezeka na kuleta
tija kwa jamii.
Alisema uamuzi wa Serikali wa kuanzisha Idara ya uhakiki wa
chakula pamoja an ghala la Akiba la chakula ni muhimu , kwani
pamoja na mambo mengine utapunguza mfumko wa bei na
kuondokana na hatari ya kuibuka kwa njaa.
Alisema Wizara hiyo kwa mashirikiano na Wizara ya Elimu na
Mafunzo ya Amali imejidhatiti kuendelea kutoa elimu kwa
wananchi katika sekta za kilimo, mifugo na uvuvi juu ya lishe bora
pamoja na matumizi endelevu ya rasilimali zilizopo, sambamba
na kuwataka wananchi, hususan vijana kutumia maonesho hayo
kupata ujuzi.
Nae, Katibu Mkuu, Wizara ya Kilimo. Maliasili, Mifugo na Uvuvi,
Maryam Juma Abdalla alisema maonyesho hayo ni ya pili
kufanyika katika eneo hilo la Chamanangwe, yakiwa na lengo la
kuhamisha wananchi na wadau kutekeleza sera za kuimarisha
kilimo nchini.
Alisema sekta ya kilimo imekuwa na mchango mkubwa katika
kukuza uchumi na mandeleo ya Taifa na kubainisha katika
mwaka uliopita wa 2018, sekta hiyo ilichangia wastani wa asilimia
21.3 ya pato la Taifa.
Alisema maonesho ya mwaka huu yameshirikisha wadau 207
kutoka taasisi za serikali na binafsi, wafanyabiashara pamoja na
watoa huduma kutoka serikalini na sekta binafsi.
Maryam aliyapongeza mashirika ya ndani na yale ya Kimataifa
kwa kuiunga mkono Serikali katika juhudi zake za kuimarisha
kilimo pamoja na kufanikisha vyema maonesho hayo.
Katika hiyo, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein alikabidhi zawadi kwa vikundi
mbali mbali vilivyofanya vizuri pamoja na kutembelea mabanda
ya maonesho kuona uzalishaji wa bidhaa mbali mbali.