NA MWAMVUA MWINYI,KIBAHA
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimekabidhi mabati 500 kwa ajili ya kuunga mkono kampeni ya ELIMISHA KIBAHA.
Kampeni hiyo inalenga kujenga madarasa ili kukabiliana na changamoto ya upungufu wa madarasa 65 unaoikabili wilaya hiyo.
Akimkabidhi mabati hayo ,mkuu wa wilaya ya Kibaha Assumpter Mshama ambaye ndiyo muasisi wa kampeni hiyo, Katibu Itikadi na Uenezi wa CCM ,Humphrey Polepole alisema, waliweka ahadi ya kuchangia mabati 600 na wameanza na mabati 500 na awamu ya pili tutatoa mabati 100 na mifuko ya saruji .
Alieleza, ubunifu huo unalenga kushirikiana na serikali na inatekeleza ilani ya chama ambayo inatekelezwa na Rais ya kutoa elimu bila ya malipo kwa shule za msingi na sekondari.
“Tangu Rais Dk John Magufuli alivyotangaza elimu bure kumekuwa na ongezeko kubwa la wanafunzi zaidi ya mara tatu na hivyo kuongeza mahitaji ya uhaba wa madarasa, madawati na walimu ambalo serikali inalifanyia kazi”
Polepole walishaongea na Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali ya Mitaa (TAMISEMI) ili kuangalia namna ya Kibaha kupewa kipaumbele kwenye mgawanyo wa walimu.
“Tunataka viongozi wahamasishe umma kama ulivyofanya wewe angalia tumeokoa shilingi ngapi kwa jitihada mlizozifanya kwa madarasa 26 ya mwanzo kati ya 65 yanayotarajiwa kujengwa kupitia kampeni hiyo ambapo fedha zilizookolewa zitakwenda kusaidia wale ambao hawajaweza kufanya kama mlivyofanya nyie Kibaha huu ndiyo uongozi unaotakiwa,” .
Awali mkuu wa wilaya ya Kibaha Assumter Mshama alisema ,baada ya uzinduzi wa kampeni hiyo iliyofanyika hivi karibuni walipata vifaa na fedha vitakavyotosha ujenzi wa madarasa 26 kwa Halmashauri mbili za Kibaha Mjini na Wilaya ya Kibaha ambapo kila moja imeanza ujenzi wa madarasa 13.
Alieleza,ujenzi wa madarasa hayo umeanza baada ya wakurugenzi wa Halmashauri hizo kupatiwa vifaa vya ujenzi ili kukabiliana na changamoto ya upungufu wa madarasa 65 ambayo thamani yake ni shilingi bilioni 1.3 .
Assumpter alisema, hiyo imetokana na idadi kubwa ya wanafunzi wanaofaulu darasa la saba.