Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kiuchumi Kusini mwa Afrika (SADC) Dk. John Pombe Magufuli akihutubia wakati akifunga mkutano wa 39 wa wakuu wa nchi za SADC kwenye ukumbi wa Julius Nyerere leo Jumamosi Agosti 18, 2019 jijini Dar es salaam.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kiuchumi Kusini mwa Afrika (SADC) Dk. John Pombe Magufuli, wa pili kutoka kulia, Rais wa Namibia Hage Geingob na Mwenyekiti aliyemaliza muda wake kulia pamoja na marais wengine hawapo pichani wakisaini mkataba wa kubadilishana wafungwa kwa nchi za SADC katikati ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Profesa Paramagamba Kabudi na kushoto ni Katibu Mtendaji Mkuu wa SADC,Dr. Stergomena L. Tax.
Baadhi ya Marais wa Nchi za Jumuiya ya Kiuchumi Kusini mwa nchi za Afrka SADC wakijadiliana jambo wakati wa kufunga mkutano huo.
Marais wa Nchi za Jumuiya ya Kiuchumi Kusini mwa nchi za Afrka SADC wakiwa katika mkutano huo. wakati wa kufungarasmi leo.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kiuchumi Kusini mwa Afrika (SADC) Dk. John Pombe Magufuli, wa pili kutoka kulia, Rais wa Namibia Hage Geingob na Mwenyekiti aliyemaliza muda wake kulia pamoja na marais wengine hawapo pichani wakipiga makofi mara baada ya kusaini mkataba wa kubadilishana wafungwa kwa nchi za SADC katikati ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Profesa Paramagamba Kabudi na kushoto ni Katibu Mtendaji Mkuu wa SADC,Dr. Stergomena L. Tax.
Mkuu wa mkoa wa Katavi Comred Juma Homera akicheza ngoma ya Watatoga wakati wa ufungaji wa mkutano wa 39 wa nchi za Jumuiya ya Kiuchumi Kusini Mwa Afrika SADC leo.
……………………………………………………..
NA JOHN BUKUKU
Wakuu wa nchi 16 zinazounda Jumuiya ya Maendeleo Kusini Mwa Afrika SADC wamesaini itifaki na makubaliano mbalimbali kwa ajili ya kuanza utekelezaji. Ambapo Itifaki iliyosainiwa na wakuu hao wa nchi ni Itifaki ya viwanda yenye lengo la kuboresha mazingira ya kukuza viwanda viweze kuzalisha vya kutosha na katika ubora unaoweza kushindana duniani.
Wakuu hao pia wamesaini Itifaki ya kubadilishana wafungwa miongoni mwa nchi wanachama itakayowezesha wafungwa waliohukumiwa nje ya nchi zao kwenda kutumikia kifungo ndani ya nchi zao.
Aidha walisaini pia makubaliano ya kurekebisha sheria za nchi zao ili kuendana na Itifaki zilizosainiwa pamoja na makubaliano ya kusaidiana katika mambo ya uhalifu.
Itifaki hizo zimesainiwa wakati wa kufunga mkutano wa 39 wa Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Kiuchumi Kusini mwa Afrika SADC uliofanyika kwa siku mbili jijini Dar es Salaam ambapo pamoja na mambo mengine wakuu wa nchi 16 zinazounda jumuiya hiyo wamesaini itifaki na makubaliano mbalimbali kwa ajili ya kuanza utekelezaji.
Akizungumza katika wakati akifunga mkutano huo Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) Rais Dk John Magufuli ameisisistiza Sekretarieti ya SADC kutumia fedha wanazopata vizuri badala ya kuishia kuzitumia katika warsha, semina na mikutano.
Rais alipendekeza Sekretarieti hiyo ione umuhimu wa kuanza kutumia fedha hizo katika masuala ya maendeleo kama vile ya elimu, afya na miundombinu.
“Bajeti ya Jumuiya yetu inafikia Dola milioni 74 lakini kituo cha afya kinagharimu Sh milioni 400 hadi 500 sawa na dola 200,000 ambazo zipo ndani ya uwezo wa sekretarieti, ” alisema Rais Magufuli.
Rais Magufuli pia amesema katika mkutano huo wamepitisha kauli mbiu itakayotumika mwaka mzima ambayo inasisitiza ujenzi wa viwanda endelevu vitakavyoongeza ufanyaji biashara na kukuza ajira.
Kauli mbiu hiyo inasema, “Maendeleo endelevu ya viwanda kuongeza ufanyaji biashara na kukuza ajira,”
Rais Magufuli amesema katika mambo waliyoazimia wamehimizana nchi wanachama kuahkikisha zinajenga miundombinu wezeshi ili kuweza kusaidia kukuza uchumi wa nchi hizo pamoja kuboresha sera za uchumi na fedha.
Aidha amesema mambo mengine waliojadili katika mkutano huo ni ombi la nchi ya Burundi kutaka kuingia SADC ambapo walijiridhisha kuwa bado kuna mambo ambayo hayajafanyiwa kazi na kuagiza sekretatieti kuwapa taarifa hiyo na baadae kwenye kuchunguza kama mambo hayo yamefanyiwa kazi.
Akizungumza kuhusu suala la vikwazo vya kiuchumi kwa nchi ya Zimbabwe Rais Magufuli amesema wamekubaliana waendelee na mazungumzo na jumuiya za kimataifa ili kuangalia namna ya kuondoa vikwazo hivyo.
Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Sekretaieti ya SADC, Dk Stergomena Tax mkutano huo umekubaliana kuwa Oktoba 25 mwaka huu itakuwa siku ya kutoa wito kwa jumuiya za kimataifa kuondoa vikwazo dhidi ya Zimbabwe.