Chaneli ya TBC ya Tanzania kuonekana katika nchi za SADC ili kuwawezesha wananchi wa nchi hizo kushuhudia mubashara mkutano wa Kilele wa 39 wa SADC
Dar es Salaam, Tanzania; 16 August 2019 – Katika kuhakikisha kuwa wateja wake wanafuatilia habari za mambo yote muhimu yanayowahusu, MultiChoice Africa imeamua kuonyesha mubashara Mkutano wa kilele wa 39 wa SADC unaoendelea katika ukumbi wa mikutano wa Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es Salaam. Kwa uamuzi huu, wateja wa DStv katika nchi za SADC sasa wanashuhudia maendeleo ya mkutano huo mubashara kupitia Shirika la Utangazaji Tanzania – TBC.
DStv sasa imefungua chaneli ya TBC kwenye soko lake la SADC kwa siku tatu kuanzia 16 Agosti hadi 19 Agosti 2019 ambapo wateja wote wa DStv katika nchi hizo wataishuhudia TBC kupitia DStv Chaneli 199 na hivyo kufuatilia moja kwa moja yanayojiri katika mkutano huo.
Mkurugenzi Mtendaji wa MultiChoice Tanzania Jacqueline Woiso amesema kuwa kutokana na uhusiano mzuri na Serikali ya Tanzania, na kwa kuzingatia uzito wa mkutano huu unaofanyika hapa nchini kwetu, MultiChoice imeamua kutenga chaneli maalum kwa nchi za kusini mwa Africa ili kuwezesha kurushwa mubashara kwa matangazo ya mkutano huo kupitia chaneli yetu ya Taifa – TBC. “Kwa kuwa tuna mtandao mkubwa kote barani Afrika tumeamua kwa makusudi kabisa kushirikiana na shirika letu la utangazaji TBC kurusha mubashara matangazo haya katika nchi zetu za SADC”
“Uamuzi huu ni ushahidi tosha kuwa ushirikiano wetu na serikali kupitia TBC umeleta matunda makubwa kwani hivi sasa mamilioni ya watu katika nchi za SADC wanaweza kushuhudia mubashara tukio hili muhimu. Hii ni sifa kubwa kwa nchi yetu” alisisitiza Jacqueline.
Kwa upande wake, Msemaji Mkuu wa Serikali Dr. Hassan Abbasi, amesema kuwa Serikali kupitia TBC ambayo inarusha mubashara mkutano huo muhimu inafurahi kuona kuwa kwa kushirikiana na wadau imefanikisha kuoneshwa kwa mkutano huo katika nchi zote za SADC kupitia TBC ndani ya DStv.
Mkutano kama huu hufanyika mara moja kila mwaka na unahusisha wakuu wa nchi wanachama na hujadili masuala ya msingi kuhusu ustawi na maendeleo ya nchi wanachama.
Chaneli hiyo maalum ya DStv ambayo itaonyesha TBC kwa nchi za Kusini mwa Africa itaonekana kupitia DStv 199 na itaonekana katika vifurushi vyote vya DStv katika nchi za Botswana, Malawi, Namibia, Africa Kusini, Lesotho, Eswatini, Zambia, na Zimbabwe.