Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Mwenyekiti wa kamati ya Baraza la Mawaziri wa SADC, Profesa Palamagamba Kabudi akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kufunga mkutano wa Baraza hilo wa siku tatu uliokuwa ukifanyika kwenye ukumbi wa Julius Nyerere jijini Dar es salaam.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi amesema Tanzani imepata heshima ya pekee kwa hatua ya Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kukubali kukiidhinisha Kiswahili kuwa lugha rasmi ya jumuiya hiyo.
Akizungumza wakati wa kuhitimisha kikao cha siku mbili cha mawaziri hao, Profesa Kabudi ambaye kwa sasa ni mwenyekiti wa kamati ya mawaziri wa SADC kwenye mkutano wa 39 unaoendelea jijini Dar es Salaam alisema hatua hiyo ni heshima ya pekee kwa Tanzania, ambayo imefanya akzi kubwa katika ukombozi wa n chi za Kusini mwa Afrika.
“Tunawshukuru mawaziri wa Sadc kwa maamuzi mliyochukua kuikubali lugha ya Kiswahili ambayo ni lugha ya ukombozi, ambayo wapigania uhuru wawe wa Frelimoi, wawe wa Swapo, wawe wa Zani-PF, wawe wa ZAPU, wawe wa ANC, PAC au MPLA waliitumia.
“Mumekubali kuwa ndiyo lugha waliyoitumia kujifunza mbinu za kivita na mbinu za medani, kisha kukabiliana na wakoloni wa Kireno, kukabiliana na utawala ubaguzi wa rangi wa makaburu Afrika Kusini na kukabiliana na Ian Smith na leo mataifa yao yako huru,” alisema.
Alisema kwa hatua hiyo, japokuwa uamuzi huo wa mawaziri unasubiri kupitishwa kwenye kikao cha marais kitakachofanyika Agosti 17 na 18, wamempa heshima kubwa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere ambaye alikifanya Kiswahili kuwa lugha ya ukombozi, kwa kukubali kukifanya rasmi kuwa lugha maalumu ya SADC, baada ya Kiingereza, Kifaransa na Kireno.
Profesa Kabudi alisema katika hatua nyingine, mawaziri hao kw apamoja wamekubaliana kuwa upo umuhimu wa kuhakikisha vikwazo ilivyowekewa Zimbabwe na baadhi ya mataifa vinaondolewa kwa sasa, kwa kuwa tayari hali ya nchi hiyo imeshabadilika.
“Tumekubaliana kuwa katika mwaka huu ambao Tanzania inakuwa mweyekitio wa SADC, tutasimamia kuondoa vikwazo kwa Zimbabwe ambayo inakabiliwa na vikwazo kutoka kwa baadhi ya mataifa, kwa kuwa tayari mambo yameshabadilika na uchaguzi umeshafanyika kwa hiyo haina sababu ya kuendelea kuwepo,” alisema
Alisema kuwa vikwazo hivyo vinasababisha taabu kwa wanawake na watoto hivyo tumependekeza kuwa vikwazo hivyo viondolewe, kwa kushirikiana na Umoja wa Afrika kuihimiza jumuiya ya kimataifa.
Picha mbalimbali za Mawaziri wa nchi za SADC wakiwa katika mkutano huo wakati ulipokuwa ukifungwa rasmi leo baada ya kufanyika kwa siku tatu.