NA MWANDISHI MAALUM – ORCI
WATU 481 wamejitokeza kupima Afya zao kutambua Iwapo wamepata maambukizi ya virusi vya homa ya ini katika Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI).
Akizungumza na waandishi wa habari mapema leo, Mkurugenzi wa Idara ya Huduma za Kinga ya Saratani Ocean Road, Dk. Crispin Andrew Kahesa amesema idadi hiyo imeongezeka kutoka watu 150 ilivyokuwa jana.
Dk. Kahesa alikuwa akizungumza kuhusu kambi maalum ya uchunguzi wa virusi vya homa ya ini bila malipo iliyoanza kufanyika Julai 27 ambayo itamalizika Julai 31, mwaka huu.
Amesema kambi hiyo inafanyika ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Homa ya Ini Duniani inayofanyika Julai 28, kila mwaka, kauli mbiu mwaka huu ikisema ‘Tafuta mamilioni ya watu wenye maambukizi ya homa ya ini’.
Dk. Kahesa amesema kauli mbiu hiyo inalenga kila nchi kuhakikisha inawatambua watu wenye maambukizi ya homa hiyo ili wapate matibabu na kuwapa chanjo wale wasio na maambukizi ili kuwakinga.
Dk. Kahesa amesema kati ya watu wote 481 waliochunguzwa katika kampeni hii hadi sasa ni watu 18 wamekutwa na maambukizi.
“Mwitikio ni mkubwa kwa kundi la wanawake kuliko wanaume, nawasihi wanaume wenzangu nao wajitokeze kuchunguza, tumekusudia kuchunguza watu 1,000,” ametoa rai.
Ameongeza “Tangu mwaka 2018 ORCI ilipoanza kufanya uchunguzi na kutoa chanjo dhidi ya ugonjwa huo, wameona watu wapatao 7,000 na 279 sawa na asilimia 3.9 kati yao walikutwa na maambukizi.
“Hii inamaanisha katika kila watu 100 nchini watu wanne wamepata maambukizi ya ugonjwa huu, aidha, takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO), zinaeleza kila mwaka watu wapatao milioni 10 duniani hugundulika kupata maambukizi kila mwaka,” amesema.
Ameongeza “Hii inamaanisha kwamba watanzania wapo hatarini kupata maambukizi ya homa ya ini, virusi hivi vinaenezwa kwa njia mbalimbali hasa kupitia mfumo wa maisha.
“Kwa mfano kugusana na majimaji ya mwili kama damu, kutoka kwa mama (mwenye maambukizi) kwenda kwa mtoto wakati wa kwa njia ya mama kujifungua, kushirikiana vitu vyenye ncha kali kama sindano, viwembe na hususani wale wanaotumia dawa za kulevya, kujamiiana pasipo kutumia kondomu.
“Ndiyo maana tunatoa rai kwa jamii waje tuwafanyie uchunguzi ni vizuri kugundua mapema na kuanza tiba kuliko kuchelewa ,” na wale ambao hawana maambukizo wahakikishe wana pata chanjo tatu amesisitiza.