Home Mchanganyiko MHE ESTHER MATIKO AKABIDHI MIFUKO YA SARUJI UJENZI WA CHOO CHA WANAFUNZI...

MHE ESTHER MATIKO AKABIDHI MIFUKO YA SARUJI UJENZI WA CHOO CHA WANAFUNZI SHULE YA MSINGI BUHEMBA

0

Mbunge wa Jimbo la Tarime Mjini Mhe Esther N. Matiko amekabidhi mifuko 20 ya Saruji kwa ajili ya ujenzi wa Choo cha Wanafunzi kitakachokuwa na Matundu 21.

Mifuko hiyo ya Saruji imekabidhiwa na Katibu wa Mbunge (Peter Magwi Michael) mbele ya kikao cha Wazazi na Walezi wa watoto wanaosoma Shuleni hapo.

Akiwa ameambatana na Mhazini wa CHADEMA Jimbo la Tarime Mjini (Esther Nyaburiri) na Mwenyekiti wa CHADEMA Kata ya Bomani Ndg Mwita Joseph (White) aliyechangia Mifuko 2 ya Saruji kuunga juhudi za Mhe Matiko kushirikiana na wananchi wake katika kujiletea Maendeleo, Katibu wa Mbunge amewahasa Wazazi hao kwa niaba ya Mbunge kujitoa kwa hali na Mali kukamilisha ujenzi wa Choo hicho ili kuhepukana na dhahama inayoweza kujitokeza kwa kufungwa kwa Shule hiyo.

Itakumbukwa kuwa Mhe Matiko alipata kufanya ziara 19/07/2019 Shuleni hapo na kujionea tatizo la Choo cha Wanafunzi kinachotumika jinsi kilivyojaa na kusababisha kuzibwa kwa Matundu mengine na kuachwa matundu 2 tu yanayotumika.

Akizungumza kwa niaba ya wazazi waliokuwa kwenye kikao hicho, Mwenyekiti wa Kamati ya Shule amemshukuru  Mhe Matiko kwa mchango wake huo na kuwaomba viongozi wengine waige mfano wa Mhe Matiko wakasaidiane nao katika kukamilisha ujenzi wa Choo hicho.

Wazazi wa Wanafunzi hao wakizungumza kwa nyakati tofauti tofauti waliokuwa kwenye kikao hicho wameuomba uongozi wa Kamati ya Shule kwenda kutafuta wadau wengine wajitokeze nao kusaidia ujenzi wa Choo hicho, “Tunaomba Mwenyekiti wa Kamati na Katibu tafuteni viongozi wengine waige mfano wa Mbunge wetu Esther Matiko, nendeni kwa Mkuu wa Wilaya, Diwani wa Kata yetu na Wafanyabiashara waje kutusaidia japo nasie tutaendelea kuchangishana kama kawaida yetu wala hatutochoka” alisema Ostadhi Ramadhani.

Katibu wa Mbunge alitumia nafasi hiyo pia kuwambia wananchi hao kuwa mchango wa Mhe Matiko wa Mifuko hiyo ya Saruji sio mwisho wa Mbunge kushirikiana na wazazi hao, “katika ujenzi wa Choo hiki tambueni kabisa Mhe Matiko ni sehemu yake, tuendelee kupeana taarifa kadri ujenzi utakavyokuwa unakwenda na Mhe Matiko hatosita kutoa kingine chochote kwa ajili ya Maendeleo ya watoto wetu” alisema Katibu wa Mbunge.